Aunty Ezekiel afunguka Haya Ya Moyoni kuhusu Kutoka Na waziri Nyalandu

Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu nchini, Aunty Ezekiel amekanusha uvumi ulioenea kuwa alikwenda nchini Marekani akifuatana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu .
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Aunty alisema hadi sasa haelewi nia ya wanaovumisha habari hiyo isiyokuwa na chembe ya ukweli wowote.
“Mashabiki wangu wajue nilikwenda Marekani kwa mwaliko wa Blogu ya Vijimambo, ambao walitaka nikashiriki katika sherehe yao ya kutimiza miaka minne, wakati wote nilikuwa na mwenyeji wangu, Lukasi Mkami,” alisema.
Mwigizaji huyo alisema akiwa Marekani alipigiwa simu na waandishi wengi wakimuuliza kuhusu ziara yake na aliwaeleza ukweli ulivyo, lakini anashangaa kibao kimemgeukia.
“Sijakaa Marekani siku 14 kama inavyoelezwa, nimekaa kule siku 10 tu, nimeenda tarehe 13 (Septemba) na kurudi 24.
Nilikutana na Nyalandu tarehe 13, Waziri alikuwa mgeni rasmi, tangu usiku huo wa hafla sikumwona tena na sijui kama aliendelea kuwapo Marekani au aliondoka.”
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Waziri Nyalandu alijibu kwa kifupi bila kufafanua alichomaanisha akisema, “Waongo wote, sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto.”
Aunty ni mmoja kati ya wasanii wa kike nchini wanaofanya vizuri katika tasnia ya filamu, ambayo imekuwa ikizidi kuitambulisha Tanzania nje ya mipaka yake kwa filamu zao tangu walipofanya mapinduzi miaka ya 2000.

Post a Comment

أحدث أقدم