Iringa/Dar. Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana kutaja siri ya chama hicho kupoteza majimbo
mbalimbali, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema chama
hicho kisahau kuchukua jimbo hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana mkoani Iringa,
Mchungaji Msigwa alisema: “Hata aje Kinana leo, nitamgaragaza hadi aone
aibu kuondoka...Mwakalebela hana ubavu wa kusimama na mimi jimboni, aje
na huyo Kinana, watakimbia.”
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Frederick
Mwakalebela alishinda kura za maoni ndani ya CCM Iringa Mjini, lakini
jina lake likakatwa katika vikao vya juu vya chama hicho.
Msigwa alisema kudhani CCM ndiyo wenye jimbo, ni
upuuzi kwani hata Mwakalebela alipata kura chache za maoni
ikilinganishwa na yeye, huku akisema Mwakalebela ‘alibebwa’ na magazeti.
“Wananchi walimchagua mtu sahihi ambaye ni
mimi...na kwamba wasimame wote hao, halafu mimi niwe mwenyewe, wataona
aibu nitakavyowashinda,” alisema Msigwa.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Uwanja wa Mwembetogwa, Kinana alisema: “Chadema wasidhani wana wanachama
hapa, CCM tumejua sababu zilizotufanya tupoteze majimbo kadhaa likiwamo
hili la hapa Iringa Mjini.”
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya Chadema,
inatarajia kukutana Dar es Salaam katika kikao maalumu kujadili mambo
mbalimbali, likiwamo la mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya
Habari Chadema, Tumaini Makene ilisema kikao hicho kitakuwa cha siku
mbili. Kikao hicho kitakuwa cha pili baada ya kile kilichofanyika
Septemba 16 mwaka huu.
إرسال تعليق