News Updates: - Taarifa ya Jeshi la Polisi ajali ya Mtumbwi (Mashua) Kigoma, 10 Wapoteza Maisha - Picha zipo Hapa


 Vifaa Vya Uokoaji Vilivyotumika Katika Shughuli hii iliyoleta Majonzi Makubwa Kwa Wananchi wa Kata ya Kagongo na Kigoma Kwa Ujumla
picha hapa ni siku ya kwanza jana(juzi) Oktoba11 huyu akiwa ni miongoni mwa waliookolewa,Mariam Maduwa (18), Bibi harusi aliyenusurika kifo kwenye ajali ya mitumbwi katika Ziwa Tanganyika, akiwa amelazwa Hospitali ya Maweni, ambapo anaendelea na matibabu....hii ilikuwa ni taarifa ya jana siku ya kwanza Oktoba11...

Watu watatu wakiwemo Watoto wawili, wamekufa maji na wengine 11 kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, baada ya mitumbwi miwili waliyokuwa wakisafiria kutoka Kijiji cha Kalalangabo kwenda Kijiji cha Kigalye kuzama katika Ziwa Tanganyika.

Tukio hilo limetokea jana Octoba 11, majira ya saa nane mchana, katika eneo la Kalarangabo wakati watu hao wakitoka harusini katika Kijiji cha Mwandiga Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenda Kigalye kabla ya mitumbwi yao kupigwa na mawimbi na kuzama umbali wa mita 200 kutoka nchi kavu.

Bibi harusi aliyetambulika kwa jina la Mariam Maduwa mwenye umri wa miaka 18, ni mmoja kati ya walionusurika kifo baada ya kuokolewa na mumewe Ramadhani Hamisi, na miongoni mwa waliolazwa katika hospitali ya Maweni kwa matibabu.

Mwingine aliyenusurika ni Rashid Jacob ambaye hata hivyo amepoteza mtoto wake katika ajali hiyo huku mkewe akiwa amelazwa hospitalini; alisema mitumbwi yao ilizidiwa na idadi ya watu waliokuwemo.

“Watu walikuwa wengi, mitumbwi ikazidiwa uwezo ndo ikawa imezama,”alisema Jacob na kuongeza kuwa: “kama kungekuwa na barabara tungesafiri kwa barabara lakini njia za huku kwetu usafiri wetu ni wa maji tu.”

Nae mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya Maweni, Bi.Amina Ramadhani mwenye umri wa miaka 48, anaelezea tukio hilo kuwa baada ya mitumbwi kuzama kila mtu alikuwa akihangaika kuokoa maisha yake ndipo ukaja mtumbwi mwingine kuwaokoa ambapo alimshukuru Mungu kwa kunusurika kifo.

Afisa Muuguzi Msaidizi katika Hospitali ya Maweni, Tatu Simba, amesema hadi kufikia jana majira ya saa tisa alasiri, walikuwa wamepokea miili ya watu watatu, majeruhi 11 waliolazwa wodi namba tano.

“Katika hao kumi na moja, wagonjwa kumi wanaendelea vizuri, lakini mgonjwa ndo hali yake sio nzuri sana na tunaendelea kuwahudumia,”alisema Bi.Simba.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma inasema watu 27 waliokolewa ingawa inahofiwa bado kuna miili ya watu wengine haijapatikana, ambapo Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, ACP Jafari Mohamed, amesema shughuli ya uokoaji inaendelea sambamba na kuchunguza tukio hilo.

“Bado tunafuatilia na kuchunguza kwa sababu hatujui watu wangapi walichukuliwa kwenye mitumbwi,na walipandia sehemu ambayo sio kituo rasmi, lakini walikuwa wengi na walikuwa wanatoka kwenye sherehe ya harusi,”alisema Kamanda Mohamed.

Marehemu aliyetambulika ni Salama Juakali, mwenye umri wa miaka 37, mkazi wa Mwandiga.

 Mashua ya Polisi ikiweka tayari kwa ajili ya kuingia majini kutafuta miili mingine leo Oktoba12 ikiwa ni siku ya pili tukio hili kutokea.
Wanajeshi wa JWTZ wakiwa wameleta miili katika mwalo wa Kararangabo ili ndugu kuwatambua ndugu zao
 Polisi wa JWTZ wakipeleka miili ya wapendwa wenzetu katika hema maalumu ili kutambuliwa na ndugu zao
 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wapili kushoto alievaa suti akisaidiana na Polis wa JWTZ katika shughuli ya kusaidi kupeleka miili ya ndugu zetu na wana kigoma wenzetu
Ndani ya Hema kwa hatua zaidi ya kutambuliwa na dugu na jamaaa
Miili ya watoto wawili waliotambulika kwa majina:-Hawa Gamba mkazi wa kijiji cha Mtanga (8) na Mahamudu Ulimwengu Mkazi wa Kijiji cha Kibirizi wakiwa wameokolewa leo Oktoba12 ikiwa ni siku ya pili ya tukio.
 Mwili wa Hawa Gwampote mkazi wa kijiji cha Mtanga (70)
Mara baada ya tukio la uokoaji Viongozi wa Mkoa walipata fursa ya kuongea na Wananchi wa Kijiji hiki Cha Kalalangabo katika kata ya Kagongo juu ya tukio hili
 Ikiwa ni siku ya pili leo Oktoba12 kutokea ajali mbaya iliyohusisha mitumbwi miwili kuzama ikiwa na watu zaidi ya 60,hapa ni mkuu wa Mkoa wa Kigoma kanali mstaafu Issa S.Machibya wapili kushoto akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kalalangabo waliokuja leo hii kwa lengo la kuitambua miili ya ndugu zao katika ajali ya mitumbwi iliyotokea jana Oktoba11,mkuu wa mkoa ametangulia kuwapa pole ndugu waliopoteza ndugu zao  katika ajali hii,pia amewataka wananchi kuacha kutumia vyombo vya usafiri ambavyo haviruhusiwi kisheria kubeba abiria,na amewataka wamiliki wa mashua zilizofanya ajali ikiwa ni pamoja na dereva muhusika kujisalimisha katika vyombo vya Dola mapema iwezekanavyo.
 mashua (Mtumbwi) kama hii ndio iliyotumika katika kusafiria watu hawa waliopata ajali,na jinsi unavyoiona hapa katika picha ndivyo inavyotumika,katikati hapo huwekwa mti maalumu ili kuishikamanisha tayari kwa safiri,kwa mujibu wa Sumatra ni kinyume na sheria za majini kwani mashua hii hairuhusiwi kusafirisha abilia kwani hii ni mashua nikwa ajili ya kuvulia samaki tu.
...mara baada ya mkuu wa mkoa kuongea na wananchi nae m/kiti wa kamati ya ulinzi na usalama Ramadhani Maneno wakwanza kulia alisema:-pamoja kuwa ziwa hili linakina kilefu kwa mujibu wa wazoefu wa eneo hili sisi kama serikali ya mkoa tutatumia mbinu zote kwa vifaa tulivyonavyo na waokoaji wetu  kuhakikisha miili yote inapatikana na istiriwe na ndugu zao,
 akijibu swali la mwandishi lililohoji juu ya mkanganyiko wa kutokujuwa na idadi kamili ya wahanga,m/kiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa amesema zoezi hili linaendelea hata hiyo kesho Oktoba12 na kama alivyosema Mkuu wa Mkoa awali kuwa watu hawa walitumia vyombo vya usafiri visivyokuwa rasmi ikiwa ni pamoja na eneo lenyewe la kupandia (Mwalo) hivyo imekuwa ngumu kupata idadi rasmi ila tunawaomba wananchi ambao wanahisi pengine ndugu zao walishiriki katika sherehe hii na hawaja waona mpaka sasa kwenda polisi kwa ajili ya maelekezo zaidi.mpaka hatua ya mwisho leo Oktoba12 kumalizika miili (Maiti) zilizookolewa jumla ni kumi (10),Watoto watano (5) na wakubwa watano (5) idadi hii inajumuisha na ile ya jana.
Nikiripoti toka eneo la tukio mimi @Eliud M.Sabuhoro picha hapo juu.

Post a Comment

Previous Post Next Post