DSC01334
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, akizungumza kwenye ufunguaji wa warsha ya wadau kujadili rasimu ya mwisho ya taarifa ya mpango wa usimamizi na uendelezaji wa pamoja wa rasilimali za maji wa bodi ya maji ya bonde la kati, liyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aquar Vitae hotel mjini Singida.
Na Abby Nkungu, Singida
MKUU wa mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone alilazimika kumtaka mshereheshaji katika Warsha ya Wadau wa Rasimu ya Mpango wa Usimamizi na Uendelezaji wa pamoja wa Raslimali za Maji Bonde la Kati kuacha kuendesha utambulisho wa wajumbe hao kwa  lugha ya kiingereza badala yake atumie Kiswahili.
Dk Kone alilazimika kuingilia kati baada ya kushuhudia baadhi ya wajumbe waliokuwa wakitambulishwa na kutakiwa kusimama ili waonekane kushindwa kufanya hivyo kwa kile kilichodhihirika wazi kupigwa na bubumbuwazi na utambulisho huo wa lugha ya kiingereza.
Akionesha wazi kukerwa kwake na mshehereshaji huyo, Dk Kone alisema kuwa wakati taifa liko katika juhudi za kukuza Kiswahili nchini, baadhi ya Watanzania wanakwamisha juhudi hizo kwa sababu hafifu kama za kuwepo baadhi ya washiriki wasiojua kiswahili.
“Wajumbe wa Warsha hii wako 200 na wasioelewa Kiswahili ni wanne tu. Idadi hii ndogo haiwezi kusababisha mkutano huu uendeshwe kwa kiingereza. Wengi wetu hapa japo tunajua kiingereza, baadhi yetu mwaka umepita bila kukizungumza; hivyo  inahitaji mtu kujiandaa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kukizungumza” alisema.
Aidha, alisema kuwa endapo Warsha hiyo ingeendeshwa kwa lugha ya kiingereza, wachangiaji wa Rasimu hiyo wangekuwa wachache hivyo kuwanyima wengi fursa ya kutoa mawazo yao.
DSC01329
Baadhi ya wadau waliohudhuria warsha ya wadau kujadili rasimu ya mwisho ya taarifa ya mpango wa usimamizi na uendelezaji wa pamoja wa rasilimali za maji wa bodi ya maji ya bonde la kati,iliyofanyika mjini Singida(Picha na Nathaniel Limu).
Katika hotuba yake ya ufunguzi Dk Kone aliwataka wadau wote kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili usimamizi wa raslimali za maji kutokana na suala hilo kuwa mtambuka. Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni migogoro inayohusiana na maji pamoja na siasa.
Alisema kuwa sekta ya maji ina jukumu kubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi lakini kwa bahati mbaya inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo bila kutatuliwa huathiri utekelezaji wa mipango na mikakati ya maendeleo na usimamizi wa raslimali za maji.
Bonde la Kati lenye makao yake makuu mkoani Singida ni miongoni mwa mabonde tisa yaliyopo nchini na linajumuisha maeneo ya Dodoma, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Arusha na Kilimanjaro ambapo linagusa jumla ya wilaya 26. Ni la pili kwa ukubwa likiwa na kilomita za mraba 143,099.
DSC01330