Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba yake wakati wa kilele cha mbio za mwenge 2014 ziilizofanyika katika uwanja wa michezo wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora siku ya jana.
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara (MB), Waziri wa Habari,
Vijana, Michezo, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu Omar Mohamedi, Waziri wa Uwezeshaji,
Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto – Zanzibar;
Mheshimiwa Fatuma A. Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Mheshimiwa Samwel Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki, Spika Mstaafu na Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar;
Makatibu Wakuu kutoka Wizara Mbalimbli Tanzania
Bara na Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa viongozi wa vyama mbalimbali vya Siasa;
Viongozi wetu wa Kiroho kutoka katika Madhebu mbalimbali;
Vijana Wetu;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nawashukuru Mawaziri wetu Mheshimiwa Fenella Mukangara wa Serikali
ya Muungano na Mheshimiwa Zainabu Omari Mohamed wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa kunialika kuja kushiriki katika sherehe za mwaka huu za
kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru. Napenda pia kutumia nafasi hii
kumpongeza na kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora na viongozi wenzake na
wananchi wote wa Tabora kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi na
kwa maandalizi mazuri. Hakika sherehe zimefana sana. Tunawashukuru kwa
mapokezi mazuri na kwa ukarimu wenu.
Pongezi kwa Wizara na Wananchi
Aidha, nawapongeza Makatibu Wakuu, viongozi waandamizi na maafisa
wa ngazi mbalimbali wa Wizara zetu mbili husika kwa kazi kubwa na nzuri
ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya Mbio za Mwenge wa
Uhuru mwaka 2014. Matunda yake mema sote tunayashuhudia na kujivunia.
Pamoja na hao napenda kuwatambua, kuwashukuru na kuwapongeza Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji wa Halmashauri na
viongozi wa Shehiya, Majimbo, Kata, Vijiji na Mitaa kote nchini kwa
kuziwezesha Mbio za Mwenge mwaka huu kupita kwa usalama katika maeneo
yao.
Mwisho, lakini siyo mwisho kwa umuhimu, nawapongeza na kuwashukuru
wananchi wote kwa jinsi walivyoupokea na kuukimbiza Mwenge katika maeneo
yao. Kama tulivyosikia Mwenge umekagua, kuzindua na kuweka mawe ya
msingi kwa miradi 1,451 yenye thamani ya shilingi bilioni 361.3. Hii ni miradi mingi yenye manufaa makubwa na kufanya mbio hizi kuwa chachu kubwa ya maendeleo hapa nchini. Hongereni sana.
Pongezi kwa Wakimbiza Mwenge
Nawapongeza sana vijana wetu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa
chini ya uongozi wa Ndugu Rachel Kasanda kwa kazi kubwa na nzuri ya
kukimbiza Mwenge kwa siku 165 kupitia Mikoa yote, Wilaya zote,
vijiji vingi na mitaa mingi kote nchini. Poleni kwa yote yaliyowakuta
lakini uvumilivu wenu na moyo wenu wa upendo na uzalendo kwa nchi yenu
ndivyo vilivyotuwezesha kufikia kuiona siku ya leo. Mwenge mmeufikisha
salama Tabora ukiwa unang’ara kama ilivyo kawaida yake. Nawashukuru kwa
Risala yenu na kwa kunikabidhi Kitabu kikubwa chenye Risala za Utii za
wananchi wa Tanzania. Kama ilivyo ada tutazisoma zote na mambo
yanayostahili kufanyiwa kazi tutachukua hatua stahiki.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo, katika sherehe hizi pia tunakumbuka tarehe na siku
kama ya leo mwaka 1999 ambapo mpendwa wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alitutoka hapa duniani. Ilikuwa siku ya majonzi na
simanzi kubwa. Leo, hata hivyo, siyo siku ya kuomboleza, bali ni siku
ya kusherehekea maisha ya kiongozi wetu mpendwa asiyekuwa na mfano wake
na muasisi wa taifa letu lililo huru la Tanganyika, Desemba, 1961 na wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964 kwa kushirikiana na Mzee
Abeid Amani Karume.
Katika kipindi cha uongozi wake na uhai wake Mwalimu aliifanyia
nchi yetu mema mengi ambayo daima hayatasahaulika. Hivyo basi, siku
kama ya leo ni ya kukumbuka kazi zake nzuri pamoja na mambo mengi mazuri
aliyotuachia kama urithi. Ni siku ya kutafakari na kuona namna gani
tutayadumisha na kuyaendeleza.
Sherehe za mwaka huu ni spesheli kweli kweli, kwani zinafanyika
siku chache tu baada ya Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi yake na
kukabidhi Katiba Inayopendekezwa. Katiba hiyo ambayo imepatikana
chini ya uongozi wa mwana Tabora, mashuhuri, Mheshimiwa Samwel Sitta
imesisitiza ubora na kuendelea kwa Muungano wa Serikali Mbili alizoasisi
Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Mzee Abeid Amani Karume. Bila ya shaka
mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyoupigania muundo huo kwa nguvu zake zote
wakati wa uhai wake. Hatuna budi kulipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa
uamuzi wake wa busara ambao unamuenzi kwa dhati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na kudumisha urithi wake mkuu kwetu ambayo ni Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Sijui tungesema nini katika Sherehe za mwaka
huu kama ndiyo tungekuwa na Katiba Inayopendekezwa yenye muundo wa
Serikali Tatu?
Mwenge na Taifa Letu
Ndugu Wananchi;
Mwenge wa Uhuru ni moja ya alama muhimu ya umoja wa nchi
yetu na utaifa wetu. Mwenge umebeba falsafa kubwa ndani yake kuhusu
nchi yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge wenye
dhiki wasiokuwa na amani. Wakati wa harakati za kudai Uhuru wa
Tanganyika kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza Mwalimu Julius Nyerere
aliwahi kusema “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya
mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale
ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima
palipojaa dharau”. Dhamira hii ilitimizwa tarehe 9 Desemba,
1961 siku Tanganyika ilipopata Uhuru. Pamoja na kupandisha bendera ya
taifa huru la Tanganyika kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge
wa Uhuru uliwashwa.
Miaka michache baadaye utaratibu wa kukimbiza Mwenge
ulianza na kuendelea mpaka sasa. Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika
nchi nzima ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na
mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano
miongoni mwa Watanzania. Aidha, Mwenge umeendelea kuwakumbusha
Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea
maendeleo yao na ya nchi yetu. Pia wapige vita maovu nchini.
Kwa kuzingatia dhima nyingine ya Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi
Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu zetu Barani
Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya
wakoloni na wabaguzi wa rangi. Ni fahari kwetu kwamba wananchi wa
Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini wamepata ukombozi
na uhuru wao na sisi tumetoa mchango muhimu. Ni jambo la faraja kubwa
kwamba nchi yetu imeweza kuwapatia hifadhi ndugu zetu wa nchi jirani na
hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya
kukosekana kwa amani au kwa kukimbia mateso ya uongozi wa kikatili na
kidikteta. Ndugu zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na
Comoro wanajua ukweli huo. Na, kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa
dikteta Idd Amin na Comoro tumewasaidia kuunganisha tena nchi yao. Hivi
karibuni ndugu zetu wa Sudani Kusini waliniomba tuwasaidie kupatanisha
makundi makuu yanayohasimiana katika Chama chao kikuu cha SPLM.
Nimekubali, hivyo tutaanzisha mchakato huo tuone tutafika nao wapi.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge
Ndugu Wananchi;
Nimefurahishwa sana na kuafiki ujumbe wa mwaka huu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unaosomeka “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi: Jitokeze kupiga kura ya Maoni Tupate katiba Mpya”.
Ujumbe huu ni mwafaka kabisa kwa kipindi hiki cha mchakato wa kupata
Katiba Mpya nchini. Pamoja na ujumbe huu mahususi wa kila mwaka, Mwenge
wa Uhuru umeendelea kuelimisha jamii na kutoa msukumo kuhusu vita dhidi
ya UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na rushwa. Nawapongeza sana
Wakimbiza Mwenge kitaifa kwa kuwasilisha ujumbe wa mambo yote manne
vizuri.
Ndugu Wananchi:
Kama mnavyofahamu nchi yetu iko katika mchakato wa kuandaa Katiba
Mpya. Mchakato huu sasa umeingia hatua ya juu kabisa baada ya kumalizika
kwa Bunge Maalum la Katiba kwa kutunga Katiba Inayopendekezwa. Baada
ya Katiba Inayopendekezwa kukabidhiwa kwangu na kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba tarehe 8 Oktoba, 2014 mjini Dodoma,
kazi inayofuata ni Kura ya Maoni ya wananchi kuamua ili nchi yetu ipate
Katiba Mpya. Hatua husika kuhusu matayarisho ya kutekeleza masharti ya
Kura ya Maoni zimeshaanza kuchukuliwa. Nawaomba Watanzania wenzangu
muwe na subira. Mtaelezwa na kuelekezwa ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimebahatika kuisoma Katiba Inayopendekezwa na naendelea kuisoma.
Kwa kweli ni Katiba bora, kuliko hii tuliyonayo sasa yaani Katiba ya
mwaka 1977. Ni Katiba inayotambua na kuimarisha tunu za taifa letu na
mambo mazuri ya huko tulikotoka na hapa tulipo. Ni Katiba
inayorekebisha upungufu uliopo sasa na kuweka mifumo mizuri inayoendana
na wakati tulionao sasa na huko mbele tuendako. Kwa lugha nyepesi ni
Katiba inayotoa majawabu sahihi kwa changamoto zetu za leo na kesho.
Katiba Inayopendekezwa inatokana na ushirikishwaji mpana wa
wananchi wa Tanzania walioko ndani na hata wale walio nje ya nchi.
Ndiyo maana haki na maslahi ya makundi yote zimetambuliwa na kupewa
nafasi yake stahiki. Kama mjuavyo, leo pia ni kilele cha Wiki ya
Vijana. Napenda mjue kuwa Katiba Inayopendekezwa imetambua haki za
vijana na kuelekeza kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Kuundwa kwa
Baraza hilo kutawaongezea vijana sauti katika kushiriki kwenye utungaji
wa sera na uamuzi unaohusu maendeleo ya vijana na nchi yenu (ambayo
ndiyo yetu sote). Kitakuwa chombo huru cha kuunganisha vijana wote
nchini bila kubagua kwa jinsia, rangi, kabila, dini, ufuasi wa vyama vya
siasa na maeneo watokako katika kutafuta majawabu ya changamoto
zinazowakabili ikiwemo tatizo kubwa la ajira.
Hii ni fursa ambayo vijana wamekuwa wakiililia tangu kutungwa kwa
Sera ya Vijana ya mwaka 1996. Hatimaye kilio hiki kimepatiwa kitambaa
cha kufutia machozi na Katiba Inayopendekezwa. Shime vijana mjitokeze
kwa wingi wakati utakapofika, mpige kura ya kuunga mkono Katiba
Inayopendekezwa ili mjitengenezee hatma njema ninyi na vizazi vyenu.
Mnayo nafasi sasa ya kihistoria ya kushika hatamu ya maendeleo yenu.
Katiba Inayopendekezwa ni fursa hiyo, hakikisheni haiwaponyoki.
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Naomba muisome kwa makini Katiba Inayopendekezwa ili muielewe na
kuona jinsi masuala muhimu kuhusu vijana na wananchi wengine
yalivyozingatiwa. Epukeni kuondolewa kwenye mambo yenye maslahi ya moja
kwa moja na ustawi wenu na kubeba agenda hasi za watu wengine. Kamwe
msikubali kutumika na kutumiwa na wanasiasa au wanaharakati kwa mambo
ambayo hayana tija kwenu na nchi yetu. Nawaomba vijana mtambue kuwa kwa
sababu ya umri wenu, ninyi ndiyo mtakaoishi na kufaidi matunda ya
Katiba Inayopendekezwa kwa miaka mingi ijayo. Kwa sababu hiyo, itumieni
fursa hii vizuri, kutengeneza mustakabali mwema kwenu na kwa vizazi
vyenu. Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwenu.
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mnajua kuwa mwezi Desemba, 2014 kwa upande wa
Tanzania Bara kutafanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Napenda
kutumia fursa hii kuwashauri vijana na wananchi wote wenye sifa stahiki
na kujitokeza kugombea uongozi. Pia nawaomba mjitokeze kwa wingi na
kushiriki kwa ukamilifu katika kupiga Kura siku ya uchaguzi. Kufanya
hivyo ndiko kutakakotupatia viongozi wazuri wanaoweza kutuvusha na
kutupeleka huko mbele kuzuri tunakokutaka. Tushirikiane ili tupate
viongozi wanaoendana na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo mbele. Ngazi
za kitongoji, mitaa na kijiji ndizo ngazi za msingi za kuanzia za
kuleta maendeleo na mabadiliko katika nchi yetu.
Shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma za jamii hasa
zinafanyika katika vijiji, vitongoji na mitaa tunayoishi. Hivyo,
mabadiliko mnayoyataka hamna budi yaanzie katika mitaa au kitongoji
unachoishi. Hii ndiyo ngazi inayotugusa moja kwa moja kila mmoja wetu
katika maisha yetu ya kila siku. Hivyo basi, vijana mjitokeze kugombea
uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Vile vile, mwakani kwenye
Udiwani, Ubunge na Uwakilishi, msibaki nyuma. Ni haki yenu na ni
wakati wenu. Gombeeni hata kwa nafasi ya Urais, na iwapo kuna mtu
anayefanana na ujana na atakuwa ametimiza masharti ya Katiba, asiogope,
ajitokeze. Watu wataamua. Shime jitokezeni mkawe chachu ya mabadiliko
katika maeneo mnayoishi na nchi nzima.
Wiki ya Vijana
Ndugu Wananchi;
Kama sehemu ya sherehe hizi, jana nilitembelea Kijiji cha
Mfano cha Vijana katika wilaya ya Sikonge. Nimefurahishwa sana na
juhudi zifanywazo na vijana za kujiletea maendeleo. Nimevutiwa na
miradi mbalimbali wanayoitekeleza pale ikiwemo ya kufuga nyuki na kuvuna
mazao yatokanayo na nyuki, ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa,
ushonaji nguo na viatu. Halikadhalika, shughuli za kilimo na ujenzi wa
nyumba bora. Nimewashauri viongozi wa Wilaya, Mkoa na Wizara waangalie
uwezekano wa kuwafanya vijana hao kuwa wakaazi na wamiliki wa eneo hilo
la miradi ili kiwe kweli kijiji cha mfano badala ya kuwa mahali pa
kupita mithili ya chuo cha mafunzo ya amali.
Baadae nitapata nafasi ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kazi
wafanyazo vijana na wadau wengine hapa uwanjani. Maonyesho haya
yanathibitisha kwa uwazi fursa zilizopo za kuwaendeleza vijana. Lililo
muhimu kufanya, ni kwa vijana kuwa na upeo mzuri wa ufahamu wa mambo,
ubunifu, moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Mkifanya hivyo
tutaondokana na tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini kwa vijana na
taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua ukweli huu, ndiyo maana Serikali zetu zimeongeza
bajeti katika Mifuko ya Maendeleo ya Vijana kupitia Wizara zetu mbili
zinazosimamia na kuratibu maendeleo ya vijana. Shabaha yetu ni
kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata mikopo na kuwa na mitaji ya
kutekeleza miradi yao itakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kujipatia
kipato. Naikumbusha Wizara inayosimamia na kuratibu Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha za Mfuko huo zinawafikia walengwa na,
kwa wakati muafaka.
Kwa upande mwingine nazikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji kutekeleza kwa ukamilifu agizo la kutenga asilimia 10
ya mapato yao kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana na
Wanawake. Ninazo taarifa kuwa baadhi ya Halmashauri zinalitekeleza
vizuri agizo hili lakini zipo nyingine ambazo zinasuasua. Nataka
isiwepo hata Halmashauri moja ya kunyooshewa kidole kwa kutokufanya
vizuri kwa jambo lenye manufaa kwa vijana wetu kama hili. Naomba
nitumie nafasi hii leo kuzitaka Halmashauri zote kutoa taarifa za mara
kwa mara za utekelezaji wa agizo hili. Taarifa ya kwanza kwa ajili hiyo
itolewe mwisho wa mwezi Desemba, 2014, ifuatayo iwe miezi minne baadae
na kila baada ya miezi minne.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
Ndugu Wananchi;
Janga la UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini
hivyo ni sahihi kabisa kwa Mwenge kuendelea kulisemea. Inakadiriwa
kuwa tunao wagonjwa wa UKIMWI milioni 1.4. Bahati mbaya waathirika wengi zaidi ni vijana. Takwimu za maambukizi zinaonyesha pia kuwa wasichana wa umri wa miaka 20 – 24 wako katika hatari ya kuambukizwa karibu mara tatu ikilinganishwa na wavulana wa umri huo huo.
Ni jambo la kutia moyo kwamba kiwango cha maambukizi kinashuka
mwaka hadi mwaka kutokana na shughuli za uhamasishaji ambazo na Mwenge
nao una mchango wake. Kwa mfano, kiwango cha maambukizi kimeshuka
kutoka asilimia 5.7 mwaka 2010 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012. Kiwango cha maambukizi ya UKIMWI hapa mkoani Tabora ni wastani wa asilimia 5.1
ambayo ni sawa na kiwango cha kitaifa. Mwelekeo huu kwa taifa na
Tabora ni mzuri lakini tusibweteke bali tuongeze bidii katika
mapambano. Watu watano katika kila 100 kuwa wameambukizwa ni wengi mno. Isitoshe maambukizi mapya 78,843 ni makubwa mno, tunataka maambukizi mapya yawe sifuri.
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita
dhidi ya UKIMWI. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaopata
tiba imeongezeka kutoka 201,181 (2005) hadi 512,555 mwaka
2013. Hali kadhalika tumewezesha huduma za kuzuia maambukizi kutoka
kwa mama kwenda kwa mtoto kutolewa karibu katika Kliniki zote nchini (aslimia 97). Vilevile, idadi ya waliopima afya zao imeongezeka kutoka watu 365,189 mwaka 2005 hadi 20,469,241 mwaka 2013. Katika mwaka 2013 peke yake, watu 2,793,636 walipima afya zao. Yote hayo ndiyo yanayochangia kupungua kwa maambukizi.
Ndugu Wananchi;
Ili kushinda vita hii hatuna budi kukumbushana kuachana
na tabia na mienendo inayowaweka wanaadamu katika hatari ya maambukizi.
Mimi naamini Watanzania tunaweza kabisa kushinda vita dhidi ya UKIMWI.
Kinachotakiwa ni kuamua kukataa kupata maradhi haya. Inawezekana,
timiza wajibu wako.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea na mapambano dhidi ya rushwa na
mafanikio yanaendelea kupatikana. Watu wengi zaidi hivi sasa wakiwemo
vijana, wamefikiwa na kampeni ya kuwafanya watambue madhila yake,
waichukie rushwa na wawe tayari kujitokeza kupambana na uovu huu.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeongeza kasi ya
kupambana na rushwa. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Juni, 2014
imefanikiwa kufungua kesi mpya 327, kati ya hizo kesi tatu ni za rushwa kubwa. Aidha, shilingi bilioni 38.96
zimeokolewa. TAKUKURU sasa imekwenda mbali zaidi na kuanzisha ofisi za
Waratibu wa Kanda (Public Expenditure Tracking System – PETS
Coordinators) wenye jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha kwenye
shughuli za ununuzi hasa kwenye miradi ya maendeleo.
Tumefanya hivyo kwa kutambua kuwa shughuli za ununuzi kwenye
Halmashauri na Serikali Kuu kwa jumla ndiko waliko mchwa wengi, wakubwa
na wanene. Katika kipindi cha 2013/14 pekee, miradi 215 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.594 imekaguliwa. Kati ya miradi hiyo, miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 9.59
ilionekana kuwa na mazingira ya mashaka na uchunguzi wa kina unaendelea
hivi sasa. Itakapothibitika kuwepo kwa dalili za rushwa, hatua
zipasazo za kisheria zitachukuliwa bila ya ajizi.
Ndugu Wananchi;
Tunaweza kupata ushindi mkubwa zaidi katika vita dhidi ya
rushwa na mafanikio tunayoendelea kupata ni ushahidi wa ukweli wa
kihistoria. Sisi katika Serikali tutaendelea kutekeleza wajibu wetu kwa
kuiwezesha TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na majengo.
Mwaka huu pekee tumeiwezesha Taasisi kuajiri Maafisa Uchunguzi na
Wachunguzi Wasaidizi 304 ili kuimarisha utendaji katika taasisi
yetu hii muhimu. Tunachohitaji ni ushirikiano wa karibu wa wananchi
katika kuwafichua wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Ukweli ni kwamba watu hao tunaishi nao katika maeneo yetu. Tuache
kuwatukuza na kuwalinda kwani kwa kufanya hivyo tunawaimarisha, na
kuwakatisha tamaa watu waadilifu na wale walio mstari wa mbele katika
mapambano dhidi ya rushwa. Tuyachukue mapambano dhidi ya rushwa kuwa ni
yetu sote na siyo ya TAKUKURU au viongozi peke yao. Ushindi dhidi ya
rushwa ni ushindi wetu sote. Hali kadhalika, kushindwa vita dhidi ya
rushwa ni kushindwa kwetu sote. Ni hasara kwako na taifa kwa jumla.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tunaendelea na mapambano dhidi ya matumizi
na biashara haramu ya dawa za kulevya. Tunaendelea kupata mafanikio
pamoja na ugumu uliokuwepo katika mapambano hayo. Wahalifu wamekuwa
wakibadili mbinu na kuongeza nguvu kila kukicha. Hata hivyo, na sisi
tumekuwa na unyumbufu wa kutosha. Ukweli ni kwamba kadri wahalifu hao
wanavyoongezeka na ndivyo wanavyoongezeka kukamatwa. Wakati katika
kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2013 walikamatwa watuhumiwa 2,000, mwaka huu tangu Januari, hadi kufikia Oktoba, (2014) watuhumiwa 6,875
wameshakamatwa na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali. Takwimu hizi
zinaonyesha namna tulivyoongeza nguvu na tunavyofanikiwa katika juhudi
zetu.
Katika Mkoa wa Tabora peke yake, washitakiwa 177
wamefikishwa Mahakamani. Kilichonisikitisha zaidi ni taarifa kuwa sasa
kilimo cha bangi kinaongezeka kwa kasi mkoani Tabora. Nawaomba
muendelee kuwa wakulima hodari wa tumbaku pekee na siyo kilimo cha
bangi.
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kuchukua hatua nyingi madhubuti kukabiliana na mtandao
wa uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, ndiyo maana taarifa za
matukio ya kukamatwa watu katika viwanja vyetu vya ndege zimepungua sana
tofauti na mwanzo mwa mwaka huu. Hii inaashiria kuwa mambo yamekuwa
magumu kwenye njia hiyo, lakini tunajua wanatafuta au watatafuta njia
nyingine. Kwa yote mawili hawatafika mbali, mkono mrefu wa sheria
utawafikia.
Tumeendelea kutoa huduma za kuwasaidia waathirika wa dawa za
kulevya kuacha kutumia dawa hizo na kurejea katika maisha ya kawaida.
Vituo vyetu vya majaribio katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na
Temeke sasa vinahudumia waathirika wapatao 1,835 kwa kutumia dawa ya
Methadone. Tanzania ni moja kati ya nchi chache sana Afrika ambazo
zimepiga hatua kubwa katika kutibu waathirika wake na wenzetu sasa
wanakuja kujifunza kwetu. Tutafanya zaidi ya tufanyavyo sasa. Nia yetu
ni kueneza huduma hiyo nchi nzima ili kunufaisha vijana wetu wengi.
Ndugu Wananchi;
Tunayo kila sababu ya kushinda vita hii. Hatamu ya
ushindi wetu iko mikononi mwa wananchi wa Tanzania na vijana ambao ndiyo
waathirika na wateja wakubwa wa dawa hizo. Kataeni kuwa mawakala wa
biashara hii haramu na ya maangamizi. Pia kataeni kuwa watumiaji wa
dawa za kulevya. Biashara hii haiwezi kushamiri iwapo hapatakuwepo na
mawakala na wateja wa uhakika. Sisi Serikalini tunaendelea kuchukua
hatua stahiki. Sasa tunapitia upya sheria ili tuweze kuanzisha taasisi
mpya yenye mamlaka makubwa ya kupambana na dawa za kulevya kuliko Tume
ya Kudhibiti Dawa za Kulevya iliyoko sasa. Maandalizi yamefikia
pazuri. Tutakamilisha jambo hili mapema iwezekanavyo.
Maji na Barabara
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza naomba niwathibitishie wananchi wa Mkoa wa Tabora
kwamba ahadi yangu ya kuleta maji mjini Tabora, Nzega na Igunga kutoka
Ziwa Victoria iko palepale. Tumechelewa kuanza kutokana na kuendelea
kutafuta fedha za kutekeleza dhamira yetu hiyo. Nafurahi kusema kuwa
Mungu ni mwema tumefanikiwa. Serikali ya India imekubali maombi yangu
na watatukopesha kiasi cha dola za Marekani milioni 264 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. Wataalamu wanamalizia michoro ya mradi ili baada ya hapo ujenzi uanze. Subira yavuta heri, wote tuwe wavumilivu.
Tunaendelea na jitihada za kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango
cha lami hapa Mkoani Tabora. Barabara zinazoendelea kujengwa
zitakamilishwa na zile zinazoendelea na maandalizi zitaanza pindi
tutakapopata fedha. Lengo letu ni kuunganisha Mkoa huu na Mkoa wa
Katavi, Kigoma na Singida kupitia Itigi hadi Manyoni. Tumezungumza na
Kuwait Fund ili watusaidie kujenga barabara ya Nyahua – Chaya wamekubali. Hali kadhalika, Benki ya Maendeleo ya Afrika wanaelekea kuwa tayari kutupatia mkopo wa ujenzi wa barabara ya Tabora - Sikonge – Koga - Mpanda.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Narudia tena kuwashukuru wote walioshiriki kwa njia moja au
nyingine kufanikisha sherehe hizi ambazo zimefana mno. Baada ya kusema
hayo natamka rasmi kwamba shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka
huu zimefikia kilele chake leo.
Nawatakia kila la kheri katika shughuli zenu za kila siku.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
إرسال تعليق