CCM, wapinzani walalamikia kasoro nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi

Katika hali isiyotarajiwa na wengi karibu viongozi wote wa vyama vya siasa wakiwamo wa Chama tawala CCM waliohojiwa kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wamelalamikia uchaguzi huo na kuainisha kasoro mbalimbali zilizochangia kuvuruga kazi hiyo yote.
Baadhi ya kasoro hizo ni pamoja na kukosekana kwa majina ya wapiga kura, majina ya wagombea kujichanganya na nembo za vyama kuwekwa tofauti.
Kasoro zingine ni kuchelewa kuanza kwa uchaguzi huo, majina ya watu kutumika kupigiwa kura na wasiohusika na mengine kuonekana katika vituo viwili tofauti.
Kutokana na kasoro hizo, CCM wanasema walilazimika kuwashauri baadhi ya vingozi wake washinikize kuahirishwa kwa uchaguzi huo kutokana na wingi wa kasoro.
CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema kwa ujumla uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi ikiwamo ya ucheleweshwaji wa vifaa katika vituo vya kupigia kura.
Anaongeza kuwa hali ilivyoonekana kuzidi kuwa na utata waliwashauri viongozi wa vyama vyao kushinikiza baadhi ya maeneo uchaguzi huo uahirishwe.
“Kwa kweli kuna dosari nyingi, kuna baadhi ya vituo vilikosa vifaa muhimu ikiwemo wino ambao sisi tuliamini ungeweza kuwadhibiti watu waliojiandikisha zaidi ya mara tatu, tulibaini miongoni mwa watu hao ni wa Chadema,” alisema.
Nnauye anasema kasoro nyingine ambayo waliibaini ni karatasi za kura zilikuwa zimegeuzwa nembo za vyama, picha na jina ni la mgombea wa CCM lakini nembo inawekwa ya Chadema.
“Pia kuna sehemu nyingine vijana wa Chadema walijipanga kwenye njia za kuelekea kwenye vituo na kuwatishia wapiga kura.
“Tatizo hilo la udanganyifu nafikiri tunaweza kulidhibiti kwa kuwa na vitambulisho vya pamoja, ingawa pia limetimia kwa sababu ya uzembe wa baadhi ya mawakala,” anasema.
Anaendelea kusema hata hivyo kuna haja kwa Serikali kuwaadhibu haraka iwezekanavyo wale wote ambao walihusika kusababisha uchaguzi kuwa na kasoro zilizosababisha vurugu katika baadhi ya maeneo.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم