Dar es Salaam. Tanzania imepoteza kiasi cha
Dola 462 milioni za Marekani (sawa na Sh794.6 bilioni) mwaka 2013
kutokana na rushwa, udanganyifu katika ankara za malipo na ukwepaji wa
kodi.
Shirika la Kimarekani la Uchumi (GFI) limetoa
ripoti mpya na kusema kuwa Tanzania imepoteza jumla ya Dola 1,762
milioni kuanzia mwaka 2011 hadi 2013.
Ripoti hiyo iliyotolewa Desemba mwaka huu,
inaonyesha kuwa Tanzania imekuwa sugu kwa kupoteza kiasi kikubwa kila
mwaka na kwa mwaka 2010, kiasi cha Dola 1,356 milioni kilipotea wakati
Dola 613 milioni zilipotea mwaka 2011 na Dola 717 milioni mwaka 2012.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la
udanganyifu katika ankara za malipo ndilo lililotawala zaidi nchini na
kusema linafanyiwa kazi na mamlaka husika.
Mkuya alisema Tanzania inapoteza fedha nyingi
zaidi kutokana na udanganyifu katika ankara za malipo ya kibiashara,
mchezo ambao umekuwa ukifanywa na raia wa China ambao ankara zao za
malipo huonyesha kuwa wameingiza mzigo mkubwa nchini lakini ukifika
katika Bandari ya Dar es Salaam, huonekana mzigo kidogo.
“Kutokana na hali hiyo, mfumo wa uingizaji wa
mizigo unaboreshwa na tutakuwa tukifuatilia idadi ya mzigo kamili kule
ulikotoka, inatushangaza kuona kinacholetwa nyumbani ni kidogo lakini
kule kimetoka kikubwa,” alisema.
Kuhusu fedha chafu zinazofichwa katika akaunti za
nje, Mkuya alisema tayari Tanzania imeshaingia katika makundi ya nchi
ambazo zitajumuika kuhakiki mifumo ya kifedha.
“Hii itatusaidia kupata taarifa za uhamishwaji wa fedha unaofanyika mara kwa mara,” alisema.
Hapa nchini zipo kesi za kampuni zinazofanya kazi
na kudai kupata hasara kwa miaka mingi na kuficha faida waliyoipata ili
kukwepa kodi.
Mapato yanavyopotea
Udanganyifu katika ankara za kibiashara ili
kukwepa kodi hufanyika mathalan, mwekezaji wa Asia aliye nchini anaweza
kununua gari kutoka Marekani kwa Dola milioni moja na anapoliingiza
huandika ankara ya uongo ya ununuzi kuwa amelinunua kwa Dola 1.5
milioni. Zile Dola milioni 5, huzipeleka katika akaunti za nje ya nchi.
Kadhalika, wahalifu hao wanaweza kutumia mwanya wa
motisha wa kodi ambao hutolewa kwa wafanyabiashara wa ndani
wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi. Wahalifu hutumia mwanya huo kwa
kuongeza idadi ya uongo ya bidhaa wanazosafirisha.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق