Baadhi ya wasomi na wanaharakati wamesikitishwa na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa ulivyokuwa na dosari zinazofanana katika maeneo mengi
ya nchi na kueleza wasiwasi wao kuwa huenda kulikuwa na njama za
kuvuruga uchaguzi huo.
wasomi
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha
(RUCU) Iringa, Profesa Gaundence Mpangala anasema uchaguzi huo umekuwa
mbaya katika maeneo mengi, lakini jambo la kushangaza dosari
zilizosababisha hali hiyo zinafanana.
“Inaonekana kwamba kulikuwa na mtandao maalumu
uliokuwa umepangwa kuvuruga uchaguzi huo kwa namna hiyo, haieleweki
ukiambiwa kwamba vifaa vinachelewa kufika katika vituo vya Dar es
Salaam,” anasema Mpangala na kuongeza:
“Bila shaka huo ulikuwa ni mkakati wa kuvuruga,
hasa baada ya kuonekana kwamba uchaguzi wa safari hii una ushindani
mkubwa ikilinganishwa na chaguzi za Serikali za mitaa zilizopita.”
Anasema kwa hali iliyojitokeza inathibitisha kuwa
Tume huru ya Uchaguzi inahitajika kwa ajili ya uchaguzi ujayo, hata kama
Katiba Mpya haitapitishwa.
Dk Banna
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Benson Banna anasema matokeo ya
uchaguzi huu yanafungua ukurasa mpya, unaonyesha dalili za wananchi
kukichoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ingawa inaelezwa kwamba CCM inaongoza, lakini
vyama vya upinzani navyo vimejitahidi kuonyesha nguvu kwa kunyakua mitaa
iliyokuwa inashikiliwa na chama tawala, vyama vinavyounda Ukawa
vimezidi kupanda hasa Chadema imechukua idadi kubwa,” anasema Banna.
Anasema matokeo hayo ni changamoto kubwa kwa CCM,
katika uchaguzi mkuu ujao mabadiliko makubwa yatashuhudiwa, hivyo hali
ya mashaka itakikumba zaidi chama hicho kama kisipojipanga vizuri.
“Pia nafikiri kwa kasoro zilizojitokeza kuna haja
ya Serikali kuona kwamba umefika wakati uchaguzi huo ukasimamiwa na Tume
ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa,” anasema.
Dk Banna anawashawishi wananchi kuwa na hali ya
uvumilivu kwa kufuata sheria mahali ambapo wanabaini matatizo badala ya
kushiriki vurugu na kusema ni busara kufanya siasa za kistaarabu.
إرسال تعليق