Hivi ndivyo ‘wazee’ wanavyopatikana mikutano na Rais

Dar es Salaam. Swali ambalo limekuwa likiulizwa kila mara Rais anapozungumza na Taifa kupitia wazee ama wa Dar es Salaam au Dodoma la jinsi gani wazee hao wanapatikana sasa limepata jibu.
Kwa muda mrefu imekuwa ikielezwa kuwa wazee hao huchaguliwa kwa itikadi za kisiasa ili kupata wale wanaounga mkono kile anachoeleza Rais.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema, “Tulitumia njia za matangazo ya televisheni, redio na magazeti kupitia habari mbalimbali. Isingekuwa rahisi kuwaalika wazee kwa njia ya barua kwani tungewaandikia wangapi?
“Sisi ambao ndiyo tulikuwa na jukumu la kuwaalika wazee hatukusema kuwa wana CCM ndiyo waje hapana, kila mmoja anaruhusiwa kuja hapa na hata uliona mwenyewe hakuna aliyekuja akazuiwa kisa siyo mwana CCM,” alisema.
Kuhusu baadhi kuvaa sare za CCM, Sadiki alisema, “Huwezi kuwaalika wazee halafu ukawapangia nguo za kuvaa, huu ni mkutano wa Rais Kikwete kama mtu anapenda kuvaa sare ya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi au chama chochote hazuiwi.
Aliongeza, “Kama chama fulani kimeshindwa kuvaa sare na kingine kimevaa huwezi kusema eti hatujawaalika, si kweli...tuache propaganda za uongo na kudai waliohudhuria ni wana CCM pekee.”
Baadhi ya wazee waliohudhuria mkutano wa jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee walikuwa wamevalia sare za CCM na kukiwa hakuna mzee au mtu mwingine yeyote aliyekuwa amevaa sare za vyama ama vya NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema au chama kingine.
Akimkaribisha Rais Kikwete kuzungumza na wazee hao, Sadiki alianza kwa kusema, “Tunakushukuru kwa kukubali kuongea na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu ulipotoka kupata matibabu.”
Sadiki alisema, “Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wanakuomba sana ukimaliza kuzungumza nao uende ukapumzike Msoga (Bagamoyo, mkoani Pwani kijijini kwake) hadi sikukuu zitakapomalizika...utuache sisi katika jiji hili lenye uzushi wa kila aina.”
Mkuu huyo wa mkoa aliendelea kusema: “wakati unakwenda kupumzika, waliomba wakupatie zawadi mbili ambazo ni ujenzi wa maabara na matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika juzi.
Matokeo
Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema katika jumla ya mitaa 555 kati ya 557 iliyofanya uchaguzi huo ulioanza Desemba 14, mwaka huu na kumalizika juzi, ni mitaa miwili tu haikufanya uchaguzi wa marudio kutokana na vurugu
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم