Tanzania yapoteza Sh800 bilioni kwa mwaka

Dar es Salaam. Tanzania imepoteza kiasi cha Dola 462 milioni za Marekani (sawa na Sh794.6 bilioni) mwaka 2013  kutokana na rushwa, udanganyifu katika ankara za malipo na ukwepaji wa kodi.
Shirika la Kimarekani la Uchumi (GFI) limetoa ripoti mpya na kusema kuwa Tanzania imepoteza jumla ya Dola 1,762 milioni kuanzia mwaka 2011 hadi 2013.
Ripoti hiyo iliyotolewa Desemba mwaka huu, inaonyesha kuwa Tanzania imekuwa sugu kwa kupoteza kiasi kikubwa kila mwaka na kwa mwaka 2010, kiasi cha Dola 1,356 milioni kilipotea wakati Dola 613 milioni zilipotea mwaka 2011 na Dola 717 milioni mwaka 2012.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la udanganyifu katika ankara za malipo ndilo lililotawala zaidi nchini na kusema linafanyiwa kazi na mamlaka husika.
Mkuya alisema Tanzania inapoteza fedha nyingi zaidi kutokana na udanganyifu katika ankara za malipo ya kibiashara, mchezo ambao umekuwa ukifanywa na raia wa China ambao ankara zao za malipo huonyesha kuwa wameingiza mzigo mkubwa nchini lakini ukifika katika Bandari ya Dar es Salaam, huonekana mzigo kidogo.
“Kutokana na hali hiyo, mfumo wa uingizaji wa mizigo unaboreshwa na tutakuwa tukifuatilia idadi ya mzigo kamili kule ulikotoka, inatushangaza kuona kinacholetwa nyumbani ni kidogo lakini kule kimetoka kikubwa,” alisema.
Kuhusu fedha chafu zinazofichwa katika akaunti za nje, Mkuya alisema tayari Tanzania imeshaingia katika makundi ya nchi ambazo zitajumuika kuhakiki mifumo ya kifedha.
“Hii itatusaidia kupata taarifa za uhamishwaji wa fedha unaofanyika mara kwa mara,” alisema.
Hapa nchini zipo kesi za kampuni zinazofanya kazi  na kudai kupata hasara kwa miaka mingi na kuficha faida waliyoipata ili kukwepa kodi.
Mapato yanavyopotea
Udanganyifu katika ankara za kibiashara ili kukwepa kodi hufanyika mathalan, mwekezaji wa Asia aliye nchini anaweza kununua gari kutoka Marekani kwa Dola milioni moja na anapoliingiza huandika ankara ya uongo ya ununuzi kuwa amelinunua kwa Dola 1.5 milioni. Zile Dola milioni 5, huzipeleka katika akaunti za nje ya nchi.
Kadhalika, wahalifu hao wanaweza kutumia mwanya wa motisha wa kodi ambao hutolewa kwa wafanyabiashara wa ndani wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi. Wahalifu hutumia mwanya huo kwa kuongeza idadi ya uongo ya bidhaa wanazosafirisha.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post