Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba.
Zoezi hilo la kujiandikisha, kuweka alama za vidole, picha na kisha kutolewa vitambulisho lilifanyika maeneo ya Bunju A na Mbweni katika Mkoa wa Dar es Salaam, Kilombero, mkoani Morogoro na Mlele katika mkoa wa Katavi.
NIPASHE jana ilitembelea katika baadhi ya vituo vya Kata ya Bunju A, Boko Magengeni, Bunju Mianzini, Mbweni Teta, na Mbweni Shule, mkoani Dar es Salaam na kushuhudia mashine hizo zinazojulikana kama Biometric Voter Registration (BVR) zikisababisha usumbufu katika uandikishaji wa wapigakura.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba (pichani), alisema changamoto zote zilizojitokeza kwenye zoezi hilo zinarekebishika na watazifanyia kazi ili zisijitokeze tena kwenye zoezi la uandikishaji wapigakura nchi nzima.
“Kwa wale ambao watakuwa hawajafanikisha kujiandikisha kwenye zoezi hili la majaribio la siku saba zoezi litakapoanza Januari mwakani, wataenda tena maeneo hayo kwa ajili ya kuandikisha, ili wapate vitambulisho kwa ajili ya kupigia kura,” alisema.
Aidha, mmoja wa wasimamizi wa kituo cha Bunju A, Agatha Moses, alisema awali zoezi hilo halikuwa gumu na mashine zilikuwa zinafanya kazi vizuri, ila kutokana na watu kuwa wengi, mashine hizo zimekuwa zikipata moto na kusumbua, hali inayosababisha watu kukaa muda mrefu bila kuhudumiwa.
Alisema uelewa wa baadhi ya wananchi ni mdogo, kwani watu wengine wasio wakazi wa kata za majaribio wamekuwa wakienda kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho na wengine kutojua sehemu walikozaliwa, yaani mikoa na wilaya.
“Kusumbua kwa mashine hizi inaweza ikatokana na sababu ya kuwa ndiyo mara ya kwanza zinatumika, na pia changamoto hizi zitaisadia NEC kuliboresha zoezi hili zaidi kwa awamu zijazo,” alisema Agatha.
Naye Sostenes Sospeter, mkazi wa Bunju A, alisema zoezi hilo ni zuri, ila mashine na makarani wa kuandikisha majina ni wachache na kuwa zimetolewa siku chache ambazo ni saba, na kusema anaamini zoezi hilo halitawafikia wananchi wote.
Salehe Mtego, Mkazi wa Mbweni Teta, alisema kituoni hapo wananchi ni wachache waliobaki bila kujiandikisha, ila tatizo lipo kwa wasimamizi wa kituo hicho, kwa kuwa mtu anayefanya kazi zote mbili ni mmoja, hali inayosababisha kuwapo foleni.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق