Katuni.
Hali hii hutikiswa kidogo wakati wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali. Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa kasoro kadhaa ambazo hujitokeza katika utekelezaji wa demokrasia ya uchaguzi, bado taifa hili siyo miongoni mwa nchi zenye rekodi ya kuwa na udikteta unaohusisha matumizi ya mabavu ya kiwango cha juu katika kuwapata watu wa kuongoza. Hakika, kwa vigezo vyovyote vile, sisi tunaamini kwamba Tanzania bado ingali na rekodi nzuri kulinganisha na maeneo mengi barani.
Wiki iliyopita, taifa lilishuhudia uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji. Wananchi walipata fursa ya kuwachagua watu wanaoamini kwamba wanafaa ili wawaongoze katika kipindi kingine cha miaka mitano. Vyama mbalimbali vyenye usajili wa kudumu na vile vyenye usajili wa muda vilipata nafasi ya kutumia nafasi hiyo kuteua wagombea wao, kuwanadi kwa wananchi na mwishowe kupigiwa kura. Mwishowe, matokeo yalitangazwa na washindi wakapatikana. Sehemu zilizobainika kwamba taratibu hazikufuatwa, au labda kulikuwa na ukosefu wa vifaa, uchaguzi huo ulirudiwa kwa mara nyingine juzi Jumapili na mwishowe maeneo mengi yakapata viongozi wao wa mitaa na vijiji.
Jambo la kushangaza, ni huku kuwapo kwa vyama vichache tu vilivyoonekana kushiriki uchaguzi huo. Mbali na Chama cha Mapinduzi (CCM), vyama vingine vilivyoonekana kujipanga kwa uchaguzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi, ACT na TLP. Vyama hivyo vilionekana kujipanga vyema. Vilishiriki uchaguzi kwa umakini na kutwaa mitaa na vijiji kadhaa. Vipo vyama vingine havikufanya vizuri sana lakini walau vilishiriki uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo nchini, baadhi vikiwa ni Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) na APPT-Manedeleo. Cha kusikitisha, vyama vingi miongoni mwa jumla ya vyama 22 vilivyopaswa kushiriki uchaguzi huo havikuonekana kujishughulisha na uchaguzi huu. Hii siyo dalili nzuri ya kuimarika kwa demokrasia. Ni ishara mbaya kwamba pengine, vipo baadhi ya vyama havina malengo ya kweli ya kutaka kuushawishi umma ili uvichague na mwishowe kukamata dola.
Bali, kadri tunavyoona, kuna vyama vya siasa vinavyotumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi wanayoyajua wao. Tunaingiwa na hofu hii kutokana na ukweli kwamba daima, chama makini cha siasa hakiwezi kuacha uchaguzi wowote wa ngazi ya mitaa na vijiji upite bila ya wao kusimamisha wagombea, tena hata wa nafasi za ujumbe katika mitaa na vijiji. Ieleweke kuwa hapa, tunachohoji siyo kila chama kutwaa viti, bali ni kutaka kuona kuwa kweli vyama vya siasa vinashiriki chaguzi za kisiasa. Kushindwa siyo tatizo, bali kushiriki na kuonyesha dhamira ya kweli ya kutaka kuwakomboa Watanzania kupitia sera mbadala walizo nazo.
NIPASHE tunashawishika kuamini kwamba vyama vya aina hii huwa havina lengo la kweli la kujihusisha na shughuli za kisiasa. Ni vyama pandikizi, ni vyama vibaraka vinavyotumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao. Daima huishia kuzungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa za kuunga mkono au kupinga mambo fulani ya kitaifa kwa minajili ya kuridhisha makundi fulani yanayowatuma.
Kwa kutambua hilo, ndipo tunapoona kwamba sasa kuna kila sababu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuvimulika vyama vyote vya siasa na kuvichukulia hatua vile visivyoshiriki siasa. Na njia mojawapo ni pamoja na kuvikagua na kuona kama kweli vina ofisi; kuchunguza ili kubaini kama kweli vina akidi inayotakiwa kisheria ya wanachama; kutambua viongozi wao na namna walivyopatikana kwa kuzingatia katiba zao wenyewe na pia, kujua kama kweli huwa vinafanya mikutano ya kujitambulisha kwa wananchi. Shime, vyama vya siasa vimulikwe ili kubaki na vyama makini vyenye dhamira ya kweli ya kutwaa uongozi wa nchi kwa nija ya sanduku la kura.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق