Kikwete aombwa kuitisha mkutano wa vyama vya siasa

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimemwomba Rais Jakaya Kikwete, kuitisha mkutano wa kitaifa wa wadau wa vyama vya siasa kabla ya kufanyika kwa zoezi la upigaji wa kura ya maoni ya katiba pendekezwa, Aprili mwaka huu.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia (pichani), amesema ili kuepusha uvunjifu wa amani kama ulivyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka jana, na kusababisha baadhi ya Watanzania kupoteza maisha, Serikali haina budi kutafuta ufumbuzi wa masuala nyeti yanayolikabili taifa, ikiwamo uundwaji wa Tume huru ya Uchaguzi, Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapigakura na kupiga stop mapendekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya kutaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) litumike kusimamia zoezi hilo.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alikuwa akizungumza juzi na wakazi wa Vunjo kuhusu mustakabali wa hali ya kisiasa nchini kwenye mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Himo,

Mkutaho huo pia ulihutubiwa na  wabunge wa Chadema, Joshua Nassari Arumeru Mashariki na Godbless Lema pamoja na  Mbunge wa Afrika Mashariki, Nderakindo Kessy.

“Serikali yetu chini ya Rais Kikwete, ifanye haraka iwezekanavyo, iitishe mkutano wa wadau wa kitaifa, tuzungumze kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na NEC kabla ya kufanyika kwa zoezi la upigaji wa kura ya maoni kwa sababu hatutaki Mtanzania yeyote amwage damu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu…Mlisikia wenzetu walipoteza maisha kule Tabora, Kanda ya Ziwa na kwingineko Desemba mwaka uliopita,” alisema Mbatia.

Alisema iko wazi kwamba, serikali imepoteza mwelekeo katika kushughulikia masuala nyeti yanayolikabili taifa ikiwamo kutekeleza pia azimio la Bunge la kumshitaki mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi.

 Kuhusu NEC kutaka uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura usimamiwe na Jeshi la Wananchi wa Tanzania huku kila Wilaya ikipangiwa kuwa na askari sita ambao watashirikiana na wataalamu wanne wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Nec pamoja na Kampuni inayotengeneza vifaa vya uandikishaji, Mbatia alisema Ukawa haikubaliani na mkakati huo na kwamba wakiulazimisha, watakuwa wametengeneza mgogoro.

“Kamwe hatuwezi kukubali JWTZ, JKT au Polisi wapewe jukumu la kusimamia uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu. Huku ni kuinyonga demokrasia na ndiyo maana tunataka mkutano wa wadau wa kitaifa uitwe haraka,” alisema Mbatia.

Akizungumzia zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba pendekezwa, Mbatia alisisitiza kwamba serikali inakabiliwa na upungufu wa dhamira ya kushughulikia mambo muhimu ya kitaifa kwa kuwa hadi sasa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hawajapewa nakala ya katiba pendekezwa ambayo itapigiwa kura Aprili mwaka huu.

“Mimi ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, sijawahi kupewa na serikali, nakala ya Katiba pendekezwa ili nitoe elimu kwa Watanzania kama wajibu wangu kisiasa …Haya basi, lakini pia kama taratibu zilivyo; kila mbunge anapaswa kupewa hiyo nakala ya katiba pendekezwa, lakini hadi leo ninavyozungumza na nyie hapa mji mdogo wa Himo, wabunge hatujapewa nakala hiyo…Sasa nyie mnaambiwa muisome muielewe, mnajua nini au mmeiona?,” alihoji Mbatia

Post a Comment

أحدث أقدم