Muswada wa Kadhi balaa, Jukwaa la Wakristo laupinga

Dar/Dodoma. Wakati mjadala mkali ukitarajiwa kuibuka katika Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza leo kuhusu uanzishaji Mahakama ya Kadhi, Jukwaa la Wakristo Tanzania limeitaka Serikali kuachana na muswada huo ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa inayopinga ubaguzi na kutofungamana na dini yoyote.

Suala la kuanzisha Mahakama ya Kadhi limo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo na unalenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya Tamko ya Sheria za Kiislamu Sura ya 375 ili suala hilo litambuliwe kisheria.

Endapo muswada huo ambao tayari umechambuliwa na wadau utapitishwa, katika sheria hiyo kutafanyika marekebisho kwenye kifungu cha tatu baada ya maneno ‘all courts’ (Mahakama zote) wataongeza maneno ‘including Kadhi Courts’ (Ikijumuishwa na Mahakama ya Kadhi).

Hata hivyo, Jukwaa la Wakristo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (CPCT) limesema mapendekezo hayo “yanaibua mambo mazito ya kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na sheria hiyo itawaathiri hata wenye imani tofauti.”

Tamko la Jukwaa hilo lililokutana Januari 20 kujadili uanzishwaji wa mahakama hiyo ni mtihani kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye Septemba 29, mwaka jana katika mkutano wa Bunge la Katiba aliahidi kuliwasilisha suala hilo katika mkutano wa Bunge unaoanza leo ili kuanza mchakato wa uanzishwaji wa chombo hicho.

Pinda alitoa ahadi hiyo kuwapoza wajumbe wa Bunge hilo kutokana na baadhi yao kuhamasishana kuipigia kura ya kukataa Rasimu ya Katiba, iwapo chombo hicho kisingeingizwa katika Katiba.

Pinda aliahidi ifikapo Januari 2015, Sheria ya Mahakimu, sura ya 11 na Sheria ya Kiislamu sura ya 375 zitafanyiwa marekebisho ili kutambua Mahakama ya Kadhi kwa lengo la kuhakikisha umoja na mshikamano vinadumu kwa Watanzania.

Wapingwa katika Kamati

Uanzishwaji wa mahakama hiyo pia uliibua mvutano mkali katika vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala wiki iliyopita na wajumbe walisema uwezekano wa kuanzishwa kwake ni mgumu.

Katika vikao hivyo, ilielezwa kuwa kati ya wadau 15 kutoka taasisi za dini, wanaharakati, wanasiasa, wanasheria na wasomi waliofika mbele ya kamati hiyo, ni mdau mmoja tu aliyekubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Miongoni mwa wadau hao ni; Islamic Propagation Centre (IPC), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, CCT, TEC, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.

Wengine ni Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (BMKT), Mwakilishi wa Kanisa la Wasabato (SDA),  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Profesa Abdallah Safari na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Post a Comment

أحدث أقدم