Dar es Salaam. Baada ya kusubiri kwa muda wa wiki mbili ili
wajumbe serikali ya mtaa wa Migombani-Segerea waapishwe na mamlaka
husika bila mafanikio, wananchi wameamua kuwaapisha viongozi hao kwa
kutumia wakili binafsi.
Tukio hilo limetokea leo asubuhi katika ofisi za
Serikali za Mitaa zilizopo Segerea Mwisho ambalo lilijumuisha kuapishwa
kwa Mwenyekiti wa Mtaa, Japhet Albert Kembo pamoja na wajumbe watatu
ambao ni Rose Benard Mhagama, Nyangeto Flora Justin na Ramadhan Rashid
Seif.
Akizungumza baada ya kuapishwa, mwenyekiti mpya wa
mtaa huo amesema kuwa wananchi wamechoshwa na danadana wanazopigwa na
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala za kutowaapisha viongozi waliowachagua
ndiyo maana wamefikia hatua hiyo ili kuwakumbusha kutekeleza majukumu
yao kwa wakati.
“Wananchi wanahitaji huduma kutoka kwa watu
wanaowaamini lakini wanakosa imani pale uongozi wa manispaa unaposhindwa
kutekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Wamemtafuta wakili ambaye amekuja kulisimamia suala hili kisheria na
ndiyo maana zoezi limefanywa hadharani,” alisema Kembo.
Wananchi waliozungumza na Mwananchi walisema kuwa
hawaelewi kinachoendelea kwakuwa uchaguzi ulifanyika kama kawaida pasipo
dosari yoyote na matokeo yakatangwazwa huku nafasi zote zikichukuliwa
na wagombea kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Uchaguzi wetu haukuwa na matatizo na ni miongoni
mwa mitaa iliyotangaza matokeo muda mfupi baada ya uchaguzi kufanyika
lakini jambo la kushangaza ni kwamba viongozi wote waliochaguliwa
hawajaapishwa kama ilivyofanyika kwa wengine katika manispaa hii wakati
hakuna pingamizi lolote mahakamani linalozuia uhalali wa
waliochaguliwa,” alisema John Kandeo, mmoja wa wananchi walioshuhudia
kuapishwa kwa viongozi hao.
Akifafanua kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofanyika
Desemba 14, mwaka jana, Kembo alisema kuwa walikuwa wagombea watatu
katika nafasi ya uenyekiti ambao ni yeye mwenyewe aliyepata jumla ya
kura 547, Uyeka Idd wa CCM aliyepata kura 273 na Erick Mchata wa
NCCR-Mageuzi aliyepata kura 205.
Zoezililivyokuwa
Muda wa saa 05:00 asubuhi, wakili wa kujitegemea
kutoka kampuni ya mawakili ya Ame and Company, Idd Msawanga aliwasili
katika ofisi za mtaa huo na kupokelewa kwa kelele nyingi za wafuasi wa
Chadema waliokuwa wakipaza sauti zao kwa sauti kubwa za ‘Peoples…Power.’
Wakili Msawanga alianza kwa kumuapisha mwenyekiti,
peke yake, na baadaye wajumbe hao watatu kwa pamoja na kuelezwa kuwa
wajumbe wawili hawakuwepo kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Sheria ya uchaguzi inaruhusu kufanya hivi na hata
hao wajumbe wawili ambao hawapo kwa leo watakaporudi nitawaapisha…ni
suala la kutaarifiana tu,” alisema Msawanga.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق