Serikali imetangaza kukutana na viongozi wa
madhehebu ya dini ya Kikristo ili kuzungumza nao kuwaondoa wasiwasi
kuhusu muswada unaokusudia kutunga sheria itakayoitambua Mahakama ya
Kadhi nchini.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju (pichani), alisema
hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, katika viwanja
vya Bunge, mjini hapa jana.
Alisema serikali inakusudia kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini
wasiwasi uliopo kwa viongozi hao unatokana na kutouelewa vizuri muswada
huo pamoja na mahakama yenyewe.
"Tutawafikia, tutaomba kuzungumza nao ili tuweze kubadilishana
mawazo vizuri. Na bahati nzuri viongozi wa dini ni wasikivu sana kwa
sababu ndiyo walinzi wetu wa kiroho. Tukiwaomba kwenda kuwaona hawawezi
kukataa," alisema Masaju.
Alisema tayari madhehebu yote ya kidini yamekwishamkaribisha aende kuzungumza nao kuhusiana na suala hilo.
"Na mimi nitaenda na wasaidizi wangu na baadhi ya viongozi
serikalini na hata walioko nje ya taasisi za serikali kuwaambia jamani
kitu chenyewe ni hiki na hiki na hiki. Baada ya uelewa, tutabaki wamoja.
Tanzania tunatengeneza sheria siku zote hizi iwe maridhiano," alisema
Masaju.
Alisema siyo Wakristo tu, bali hata Waislamu wenyewe pia kuna mambo
mengine wamepeleka serikalini, ambayo ni makubwa zaidi yanayowapa
Wakristo wasiwasi na kusema nao pia watawafikia pamoja na madhehebu
mengine.
Alisema haoni sababu ya viongozi wa dini kutofikia nai mwafaka na kusisitiza kuwa anaamini kwamba, watakubali.
Alisema fedha za kuendesha mahakama hiyo zitaendele kugharimiwa na
Waislamu wenyewe na kwamba, suala la kwenda kwenye mahakama hiyo ni la
hiari.
Masaju alisema maandalizi ya muswada huo yameshirikisha Waislamu
kwa kiwango kikubwa na kwamba, serikali imeshauriana nao na kwamba,
mchakato huo ni wa siku nyingi, uliokuwapo tangu enzi za utawala wa Rais
mstaafu, Benjamin Mkapa.
"Hii serikali nayo ilipokuja awamu hii nao wakaendelea mpaka tukafikia hatua pal," alisema Masaju.
Aliongeza: "Kwa hiyo, Waislamu wenyewe hawa tumewa-engage kwa siku
nyingi sana kwenye hili suala kupitia Bakwata na taasisi zake. Na
Bakwata ndiyo inayotambulika kisheria. Ipo kisheria ile Bakwata. Lakini
haina maana kwamba, walikuwa wanakuja Bakwata tu Waislamu wengine
walikuwa hawaji, hapana."
“Sasa baada ya kuelewana na Waislamu ndiyo unaona hata jinsi
muswada ulivyo, wao wakaanzisha mahakama ya kadhi, sisi tunaona
inahitaji inforcement kama haitambuliki.
Ndiyo maana unaona kwenda kule liwe la hiari ya mtu na kwa Waislamu.
Alisema ana uhakika mchakato huo unaolenga kujenga maridhiano,
ukikamilika utatengeneza kitu, ambacho kitawafanya Watanzania wote
kubaki wamoja.
Masaju alisema tatizo la uelewa kuhusu muswada huo anahisi
linachangiwa na hatua kutochukuliwa mapema ili kuwaelimisha sheria
inayokusudiwa kutungwa na lengo la serikali, kwani hakuna katiba
inayovunjwa kwa kuletwa mabadiliko hayo.
Hata hivyo, alisema ana matumaini kuwa baada ya zoezi wanalolifanya
la kushauriana na makundi yanayohusika, hatimaye watafikia mwafaka na
sheria itakayotungwa itakuwa nzuri inayoridhiwa na pande zote mbili
إرسال تعليق