Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza,
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, baada ya aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo, William
Ngeleja, kujiuzulu.
Ngeleja, ambaye ni Mbunge wa Sengerema (CCM), alijiuzulu nafasi
hiyo, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kupata mgawo kutoka katika
fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alithibitisha jana bungeni, kuhusu Rweikiza kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema jana kuwa
amesikitishwa sana kumpoteza Ngeleja kama mwenyekiti wa kamati hiyo.
“Hii haina uhusiano na masuala yake ya Escrow na siyo utetezi wa
aliyoyatenda na aliyoacha kuyatenda kuhusiana na sakata la Escrow. Ubora
wake kwenye kamati siyo utetezi wa makosa yake ya Escrow,” alisema
Lissu, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
Alisema Ngeleja aliongoza kamati hiyo vizuri na kuijengea heshima
kubwa tofauti na mtangulizi wake, Pindi Chana, ambaye kwa sasa ni Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Lissu alisema chini ya uongozi wa Ngeleja walijadili miswada ya sheria na kupokea maoni ya wadau na kuyafanyia kazi vizuri.
“Na kwa sababu hiyo, quality ya taarifa za kamati iliongezeka sana
hata ubora wa maoni ya wadau uliongezeka sana. Ngeleja ameiunganisha
kamati kweli kweli. Wakati wa Chana kamati iliongozwa na mkono
usioonekana. Kilichokuwa kimezungumzwa kwenye kamati sicho kilichokuwa
kinaingizwa kwenye taarifa tofauti na wakati wa Ngeleja,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Kwa hiyo, kipindi cha Ngeleja kilikuwa kizuri sana.
Mimi nimesikitika sana kumpoteza Ngeleja kama mwenyekiti wa kamati.”
Wajumbe wengine waliomsifu Ngeleja, ni Ali Khamisi Seif (CUF), Rukia Kassim (CUF) na Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi)
إرسال تعليق