Sema magharibi ya London siyo sawa na ya Afrika Mashariki.
Majira yanapobadilika na mwangaza wa jua kutumbukia; huja na mbwembwe
zake. Tuko msimu wa baridi kali yenye barafu ukanda wa kaskazini wa
dunia. Kiza huanza kukonyeza saa tisa alasiri. Hiyo saa kumi na moja
jioni tunayosimuliana giza finyu lilishapiga deki. Mchana, kwaheri.
Lakini shughuli za wanadamu zilezile. Maduka hayajafungwa. Duka
tunalotazama ni la hawa wamachinga pembe ya barabara kuu. Wahindi wenye
maduka wanajuana kwa vilemba. Mmachinga wetu ni Mpakistani. Ana kameza
kake kadogo mbele ya upenu wa mita tano kwa mapana ya mita moja, kajaza
simu za mkononi, vibiriti, sigara. Jambo la ziada ni simu na vipengele
vyake. Betri, waya, mikebe ya kuzifungia; kila unachokililia kwa simu
yako; ongeza yeye fundi.
Iko siku aliniambia kwao alihitimu ualimu ila
sababu ya rabsha za kisiasa akatupilia mbali taaluma yake akafuata ndugu
aliowajua London. Ukimchunguza hajafikisha miaka ishirini na tano.
Yuko hapa miaka miwili. Alianza kaduka bila meza na mifuko ya plastiki.
Akiuza kadi za Lyca Mobile, kampuni ya bei rahisi inayotumiwa sana na
wageni Uzunguni. Mtanzania anapopiga simu kutoka huku mara nyingi
anatumia mtandao wa Lyca. Simu za viganjani ni biashara nzuri. Tuseme
suala zima la kompyuta na mitandao ni kitengo chenye masilahi.
Watazameni vijana wawili waliounda WhatsApp. Mmoja
kwao ni Ukraine. Walianza kitu kidogo tu lakini leo mabilionea baada
ya kumuuzia Myahudi anayemiliki Facebook uvumbuzi wao. Vijana wa
Kitanzania mnaosoma kuweni wabunifu. Jaribuni kutafiti na kujua nini
kinatakiwa. Uchunguzi wa kina badala ya domo sana na siasa za
malalamiko.
Basi, Mpakistani alichangamkia umachinga na hizo
kadi. Baada ya miaka miwili, hauzi tu vidato vya simu. Anazikarabati.
Ukimuuliza kajuaje, atakwambia alipofika Uingereza alikwenda chuo
akasomea ufundi miezi kumi. “Mengine ni utundu tu...” Kaduka hakiishi
wateja. Hula hapo hapo, kutwa, kasimama akichora fedha.
Siku hii tunayohadithiana nilitaka asafishe
mfereji wa simu yangu uliokuwa na mushkeli. Wakati nimetoa pochi
n’namlipa paundi tano alizotaka (kama shilingi elfu kumi na mbili);
kando yangu kajipachika bonge la mtu. Mwamba. Niliisikia sauti yake
nzito kabla ya kushuhudia tambo lake. Macho yanakodolea zile fedha
ninazomlipa Mpakistani.
“Nipe paundi moja nikanunue maji. Nitakurudishia.”
Kamngurumia Mmachinga. Sauti nzito. Ilinikumbusha
mchezaji fulani wa sinema. Nilipogeuka nikamaizi nimemfikia begani.
Mweusi sana. Hajavaa nguo chafu. Yuko kawaida. Kiingereza chake kina
lafudhi hakika ya Kiafrika. Mpakistani kamwambia hana hiyo paundi moja
ambayo ni kama ya shilingi elfu mbili na kitu za Tanzania.
“Nipe bwana nitakurudishia!” Jamaa kazoza, na kusonya juu.
Hapo sasa ananizonga na miye maana kanafasi
tulichosimama wawili hakitutoshi. Kawaida huku Uzunguni mteja anapokuwa
akihudumiwa, wale wanaomfuata husubiri zamu yao katika foleni. Hivyo
jamaa hajafuata utaratibu. Ongeza kiburi.
Mpakistani kapokea fedha niliyompa. Akaiweka
kibindoni. Upesi akachakura makabrasha nyuma ya bidhaa zake, akarejea
na chupa ndogo ya maji. Akampa jamaa. Bure.
“Haya chukua, maji. Hela sina, samahani.”
Post a Comment