Ukiumwa na nyoka ukiona unyasi unashtuka ,ndivyo ilivyokuwa kwa
Rhobi Pristiana Samwel (42)mratibu wa nyumba salama iliyo chini ya
Kanisa la Anglikana Mugumu Serengeti Dayosisi ya Mara.
Mwanamke anayepambana kuhakikisha watoto wa kike
wanasikilizwa na kuendelezwa kama ilivyokuwa kwa watoto wa kiume, ikiwa
ni pamoja na kuwanusuru na ukatili wa kukeketwa na ndoa za utotoni ili
wazee waweze kupata ng’ombe bila kuangalia wapi wanaenda, maisha yao
yatakuwaje.
Mwanamke ambaye anasema mateso aliyoyapata akiwa
mdogo bila kusikilizwa na wazazi wake, ndiyo yanamsukuma kupambana usiku
na mchana ili yasiwakute watoto wa kike kwa kuwa madhara yake ni
makubwa.
Nini msukumo wake
Anasema yeye alikeketwa kwa nguvu na wazazi wake
na alipata madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuvuja damu nyingi,
akapoteza fahamu kwa zaidi ya saa tatu. “Sherehe iligeuka majonzi kwa
kuwa watu walianza kulia…pamoja na kutumia dawa za jadi hazikusaidia,
”anasema kwa uchungu.
Anasema tukio hilo likitanguliwa na mwanafunzi
mwenzake aliyekeketwa awamu ya kwanza akafariki dunia na kisha maiti
yake kutupwa ni vitu vinavyogusa moyo wake na aliapa kuhakikisha
anasimama imara kutetea watoto wakike ili kuwaepusha na madhara hayo.
Rhobi mtoto wa kwanza kati ya watoto 12
waliozaliwa kwa mama mmoja anasema kutokana na tukio hilo wazazi wake
hawakuthubutu kukeketa wadogo zake 6 wa kike, hata majirani waliutumia
mfano huo kupinga ukeketaji. Hali hiyo ilimsukuma kusoma kwa bidii ili
aitumie elimu yake kusaidia wasichana waliokatika hatari ya kufanyiwa
ukatili.
Aliwekewa vikwazo kusoma
Anabainisha kuwa pamoja na kufaulu kujiunga na
shule ya sekondari akiwa msichana pekee kutoka Kijiji cha Matongo,
Buhemba Wilaya ya Butiama, ndugu akiwemo babu yake walimtaka baba yake
asimsomeshe ili apate ng’ombe wakitumia mfano wa msichana pekee katika
kijiji hicho alipata ujauzito akiwa kidato cha nne na kuonekana
wasichana hawana faida.
“Nilisoma kwa bidii nikafaulu kujiunga na kidato
cha tano,hata hivyo baba alikataa nikaenda ualimu, kisha nikajiunga na
JKT… Niliporudi nyumbani nikakuta baba amepokea ng’ombe za mtu bila
kunishirikisha, kwa kweli inauma kwa kuwa yanayoendelea sasa kuhusu ndoa
za lazima na za utotoni nami yalinikuta,” anasisitiza.
Anasema pamoja na kukataa kuingia kwenye ndoa hiyo
alitishiwa kutengwa na ndugu,mwisho akakubali kuolewa kwa sharti la
kutokufanya sherehe na mme ambaye mpaka sasa wanaishi naye, hali hiyo
ilimzidishia machungu kutafuta elimu zaidi ili aweze kufikia malengo ya
kuwasaidia watoto wa kike wanaofanyiwa ukatili.
“Pamoja na kuwa tulikuwa kijijini na mume wangu
akifundisha, nilimshawishi tuhamishie biashara yetu mjini ili nipate
fursa ya kusoma…alikubali bila kujua dhamira yangu,nikiwa nafanya
biashara nikaanza kusoma chuo kikuu huria,nilipata msaada kutoka Woman
Grant, nikahitimu shahada yangu ya biashara na utawala lakini
sikuridhika nikaendelea kusoma shahada ya maendeleo ya jamii,” anasema
- Mwananchi
Post a Comment