Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwanza nianze makala haya kwa kumshukuru Mungu kwa kutupa uzima leo. Ahimidiwe daima.Baada ya kusema hayo niseme wazi kwamba nchi yetu ilitikisika tena wiki iliyopita baada ya polisi wetu kuwapiga Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake.
Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, haitakuwa busara kila mtu kujifanyia mambo yake anayotaka bila kuzingatia sheria na hasa askari wetu.Ningefurahi kama vyombo husika vitafanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na ikibainika kuwa polisi walitumia nguvu kubwa wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Binafsi na wapenda amani wote katika nchi hii bila kujali itikadi za kisiasa tunalaani vikali kitendo cha kupiga raia kama mbwa mwitu.
Naamini yeyote aliyeona tukio lile kwa njia ya video alisikitika, alishangaa na kuingia woga kwa sababu hakuna aliyekuwa anategemea kuona askari wetu wakifanya vitendo ambavyo vilikuwa vikifanywa na askari wa Makaburu dhidi ya Waafrika kule Afrika Kusini.
Kwa nini askari umpige mtu ambaye ametii sheria au amri ya kukamatwa bila shuruti wakati huo ndiyo msemo wa jeshi la polisi?Kwa tukio hili ni lazima serikali isimamie sheria bila kupendelea mtu yeyote. Nasema hivyo kwa sababu suala la amani ya nchi ni suala la kitaifa na halitakiwi kuingizwa kwenye siasa, hivyo nawasihi viongozi wa polisi kuwa makini na suala hilo ambalo limetia doa nchi yetu.
Nasema limetia doa kwa sababu hata sasa ukifungua mitandao mbalimbali duniani ikiwemo ya Voice of America (VoA), polisi wetu wanaonekana wakiwapiga raia hata bila kujali wanapiga sehemu gani. Tumshukuru Mungu, hawakuua!
Lakini yeyote aliyeona video ile ni lazima atapata hasira kwa askari wale wachache waliokiuka sheria ya ukamataji raia waliokosa.Nisisitize tu kwamba amani na usalama wa nchi yetu ni kitu muhimu sana katika ustawi wa taifa letu, lakini kila siku tunashuhudia kuendelea kuporomoka kwa amani na usalama, ninawasihi wananchi wenzangu, tunapojadili suala kama hili lazima tuweke kando itikadi zetu, lengo likiwa kuliponya taifa.
Nisisitize kuiomba serikali kufanya uchunguzi kupitia vyombo vyake, pia bunge lichunguze sheria ambazo zinatoa mwanya wa vurugu ili kudhibiti vitendo hivyo.Suala hili ni nyeti kwa sababu limeweka bayana kugongana kwa mihimili mitatu ya nchi baada ya Bunge kujadili suala hilo wakati likiwa limeshafika mahakamani.
IGP Mangu.
Mgongano huo umetokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili baada
ya Bunge kugoma kupokea zuio la mahakama la kujadili kashfa ya uchotwaji
fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escow na kuendelea na mjadala ambao
ulifikia maazimio ya kuwawajibisha wahusika.Sitamzungumzia Profesa Lipumba juu ya kukamatwa kwake Jumanne iliyopita wakati akielekea Zakhem, Mbagala Dar kwa sababu shauri lake lipo mahakamani.Licha ya shauri hilo kuwa mahakamani, wabunge walijadili kwa kina tukio lote la kupigwa na kukamatwa kwa kiongozi huyo.
Ukweli ni kwamba Jeshi la Polisi Tanzania lilifanya haraka kuwahisha shauri hilo mahakamani na kitendo hicho wachunguzi wa habari wanasema kililenga kulizuia Bunge kutekeleza azma yake ya kujadili tukio hilo.
Jeshi la polisi halipaswi kutumia nguvu kuliko zinazohitajika katika kukamata watuhumiwa wa makosa ya jinai hilo halipo kwenye sheria naambiwa ipo kwenye maagizo ya jumla ya polisi yaani Police General Orders.
Ukweli ambao upo wazi ni kwamba sheria haiwapi polisi mamlaka ya kupiga raia anayetii sheria au amri ya kukamatwa.
Ninachoweza kusema hapa ni kuwa kilichotokea kwa Profesa Lipumba tusikichukulie kivyama bali tuangalie kwa upeo mpana wa kuendeleza amani na ushirikiano kati ya polisi na raia na mali zao.
Namshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu na safu yake ya uongozi kwamba jeshi lake liepuke kuonekana kana kwamba bado lina mfumo wa kikoloni ambao walikuwa wakikandamiza raia kwani linafanya yale yale yaliyokuwa yakifanywa wakati wa ukoloni.
Nizidi kukushauri IGP Mangu kuwa sheria za polisi zibadilishwe kwa kuwa zina mfumo wa ukandamizaji na kwamba ikibaki hivyo italiingiza taifa kwenye maafa makubwa na ni hatari polisi kuwa adui wa raia wema.
Mwisho niwapongeze wabunge wote walioona athari ya kitendo kile hasa Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba ambaye alisema hata kama serikali inaundwa na CCM, lakini si kweli yanayofanywa na dola yote ni maagizo ya chama hicho.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
إرسال تعليق