Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja.
MIMI si Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi
la Polisi kama alivyo Paul Chagonja wala siyo mwakilishi wa wananchi
wote, lakini linapokuja suala la falfasa ya uongozi ni IMANI nalazimika
kuwa Chagonja na pia mwakilishi wa wananchi wote.Kabla sijasonga mbele na makala haya naomba ninukuu kauli ya Mbunge wa Arusha Mjini aliyoitoa bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita alipomtuhumu afisa huyo wa polisi kwa uhalifu alisema hivi:
“Na mimi nikiwaambia nimelichunguza. Jeshi la Polisi limepasuka. Ma-RPC (makamanda wa polisi wa mkoa) wanalalamika. Chagonja haamini kama Rais ameshafanya uteuzi wa IGP.
“Na mimi nasema hata hizi bunduki zinaoibwa (akimaanisha kwenye vituo vya polisi na sehemu nyinginezo) inaweza ikawa mkakati wa Chagonja ku-sabotage (kumhujumu) IGP.”
Haya ni maneno machache lakini uzito wake kwa usalama wa taifa ni mkubwa mno. Ndiyo maana nikasema ningekuwa Changoja nisingepuuza kwa sababu yanaiondoa IMANI ya uongozi wangu. Hata nikiwa mwakilishi wa wananchi siwezi kukubali kuongozwa na mkusanya bunduki na mmwaga damu.
Kuwa na jeshi la polisi ambalo viongozi wake wa ngazi za juu wanatuhuma nzito kama hizi ni jambo la hatari. Wiki iliyopita katika makala yangu ya Uchochezi niliandika ufa niliouna ndani ya jeshi la polisi, mate hayajakauka usalama wa taifa unawekwa rehani na kauli kutoka bungeni.
Ni vipi Chagonja anaweza kusimamia oparesheni ilhali anatuhumiwa kuhujumu jeshi? Chagonja ataelewekaje atakaposimamia msako wa mauaji (siombi yatokee) ya wananchi yatokanayo na ujambazi wakati ametajwa kwenye listi ya ukurasa mweusi wa umwagaji damu?
Vipi jeshi la polisi linalotajwa kuwa limepasuka litaaminiwa na wananchi kwenye suala la ulinzi? Kuna mambo mawili ya kufanya kwa mustakabali wa taifa hili. MOJA; tuhuma zikithibitishwa jeshi la polisi livunjwe na kuundwa upya, na PILI mtoa tuhuma ambaye ni Lema atoe ushahidi wa alichosema.
Nasikitika; kadiri siku zinavyokwenda mihimili mitatu ya nchi kwa maana ya Bunge, Mahakama na Serikali imegeuka kuwa siyo mihimili tena bali ni nyufa zinazotishia amani ya nchi hii.
Limekuwa jambo la kawaida kinga ya kutoingiliwa kiutendaji kutumiwa vibaya na mihimili hii. Mahakama za leo zimejikuta katika tuhuma za uhalifu, serikali na bunge hali kadhalika; ukihoji utaambiwa wana kinga, jambo la kipuuzi kabisa.
Kinga ya bunge inawezaje kuwa mantiki kwa taifa kama inatumika kuyumbisha nchi? Mbunge kalala aliko lala pengine kaamka na ulevi anaingia bungeni na kutoa maneno mazito kama ya Lema halafu haulizwi, kisa ana kinga!
Itakuwaje siku rais akiamka na kuanza kuua watu kwa kutumia kinga yake? Itakuwa nchi ya aina gani pale mahakama itakapoamua siku moja tena kwa makusudi kuacha kufuata sheria na kuhukumu watu kwa hila? Itakuwaje?
Nimeandika mara nyingi hoja nzito zenye ushauri wa bure kwa serikali, sijaheshimika, badala yake nimekuwa mtu wa kupokea vitisho, eti niache kusema ninayoyaamini kwa ajili ya nchi na wananchi wenzangu.
Siwezi kukaa kimya; kama Chagonja akithibitika kuhujumu usalama wa taifa aondolewe na ashtakiwe. Na ikiwa Lema ametoa kauli ya kipuuzi bungeni asiachwe.
Nayasema haya kwa sababu najua vyombo vya usalama vipo. Kwa bahati nzuri Lema amemtaja Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe kuwa anaujua makakati wa Chagonja, nitashangaa kama ataendelea kukaa kimya. Mambo mawili lazima yafanyike; Chagonja au Lema mmoja lazima asulubiwe.
Nachochea tu!
إرسال تعليق