Daftari la Wapiga Kura Kuanza Kuboreshwa Wiki Ijayo.....Watanzania washauriwa kujitokeza kwa Wingi ili Wajiandikishe

SASA ni rasmi kwamba kazi ya kuliboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura nchini kote, itaanza Jumatatu ijayo Februari 16 na kumalizika Aprili 29 mwaka huu.
 
Uandikishaji huo utaanzia katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara na Njombe na baadaye utahamia katika mikoa mingine.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ratiba ya upigaji wa kura ya maoni ambayo ni Aprili 30 iko pale pale, kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete. Wakati uandikishaji huo ukianzia katika mikoa minne, utafungwa kwa kumalizia Dar es Salaam na Zanzibar.
 
Akizungumza jana ofisini kwake, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uboreshaji wa daftari la wapigakura baada ya utoaji wa elimu kwa waratibu kukamilika.
 
Alisema tume hiyo imetoa elimu kwa waratibu wa waandikishaji kwa kila mkoa na katika kila mkoa wametoa mafunzo hayo kwa mratibu mmoja.
 
Pia, elimu imetolewa kwa maofisa waandikishaji wa Halmashauri, na wasaidizi wao na hao ndio watakaotumika kutoa elimu kwa waandikishaji wadogo katika ngazi za tarafa na kata.
 
Masham alisema ni haki ya kila Mtanzania kujiandikisha. Alisema wananchi wana haki ya kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha ili ifikapo Oktoba mwaka huu waweze kutumia haki hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
 
“Kila Mtanzania atapata fursa ya kujiandikisha na kupata kitambulisho chake ambacho atakitumia wakati wa kupiga kura. Hivyo tunawaasa watanzania wote wanaposikia uboreshaji umefika katika eneo lake ajitokeze kujiandikisha,” alisema.
 
Katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahakikishia Watanzania kuwa uandikishwaji wa wapiga kura ambao utatumia Mfumo wa Kielektroniki (BVR), utafanyika kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
 
Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuhusu uhakika wa uandikishaji huo, Pinda alisema tume ya uchaguzi inaamini kuwa vifaa vitakavyotumika, vina ubora mara mbili ya vilivyoletwa kwa ajili ya uandikishaji wa majaribio.
 
Licha ya kukiri kuwa awali serikali ilikuwa na tatizo la kifedha, Pinda alisema tume imewahakikishia kuwa shughuli zote za upigaji kura kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, zitafanyika.
 
Pinda alimtoa wasiwasi Mbowe kuhusu ufanisi wa vifaa hivyo vya BVR, kwa kusema endapo tume itaona kuwa uandikishaji huo hauwezekani kwa sababu yoyote ile, itatoa taarifa bungeni na serikali iko tayari kubadili maamuzi

Post a Comment

أحدث أقدم