Mabweni ya Shule ya sekondari Idodi Jimboni kwa Lukuvi Yateketea kwa Moto TENA

BWENI la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Idodi iliyoko Jimbo la Isimani Wilaya ya Iringa Vijijini Mkoani Iringa, limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, ikiwa ni miaka sita tu tangu bweni hilo liungue na kusababisha hasara kubwa na vifo vya wanafunzi 13.
 
Agosti 25, 2009 bweni la shule hiyo, liliwaka moto na kusababisha vifo vya wanafunzi wa kike 13, ambao baadhi yao walizikwa shuleni hapo baada ya miili yao kuharibika vibaya.
 
Katika tukio hilo, wanafunzi wengine 23 walijeruhiwa vibaya, baada ya bweni hilo kushika moto uliosababishwa na mshumaa uliowashwa na aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Naomi Mnyali ambaye alisahau kuuzima baada ya kumaliza kusoma.
 
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani Iringa, Inspekta Kennedy Komba alisema kuwa bweni hilo limeteketea lote na kuunguza baadhi ya mali, zikiwemo za wanafunzi zilizokuwemo katika bweni hilo.
 
Alisema taarifa za awali zinaonesha chanzo cha moto huo, kilitokana na hitilafu ya umeme na kwamba hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
 
Komba alisema kuwa baada ya jeshi la zimamoto kupata taarifa ya tukio hilo, lililotokea kati ya saa 3 na 4 jana asubuhi wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa darasani, iliwachukua dakika 45 kufika katika eneo la tukio.
 
Alisema baada ya kufika katika eneo la tukio kutoka Iringa mjini ambako ni umbali wa kilometa 40, kazi ya kuuzima moto huo haikuwa kubwa, kwani wananchi waliofika kutoa msaada, walifanikiwa kuzima moto huo kwa kiasi kikubwa.
 
Aliwapongeza wananchi kwa moyo wa ushujaa wa kujitolea na kuwataka kutoa taarifa mapema pindi majanga ya moto, yanapojitokeza katika maeneo yanayowazunguka.
 
“Endapo tungepata taarifa mapema ninaamini tungeweza kuokoa vitu vingi zaidi,” alisema Kamanda huyo na kuwataka wananchi wasitegemee mtendaji au kiongozi apige simu kwa kikosi cha kuzima moto kwani kila mtu ana fursa ya kupiga simu 111 katika kitengo cha mawasiliano cha jeshi hilo kuweza kutoa taarifa ya majanga.
 
Aliongeza kuwa walitumia muda mdogo kufika eneo la tukio, kutokana na ubora wa gari walilokuwa nalo na kuwashukuru wananchi kwa taarifa na kuweza kuonyesha ushirikiano katika uzimaji wa moto huo usilete madhara zaidi.
 
Akizungumzia hasara iliyosababishwa na moto huo, Komba alisema tathmini kamili ya mali zilizoteketea, itafanywa kwa kushirikiana na uongozi wa shule na taarifa yake kutangazwa.

Post a Comment

أحدث أقدم