Simbachawene awakutanisha wawekezaji wa ndani na Serikali

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia), akimsikiliza Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi ambaye pia ni mdau katika sekta ya madini, Dk. Reginald Mengi.
Wiki moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kuchukua uongozi wa wizara hiyo, amewakutanisha wawekezaji wa ndani na serikali kuzungumzia uwekezaji kwenye sekta ya madini.
Katika mkutano uliofanyika jana jijini Dar es Salaam Waziri aliwatangazia wawekezaji hao kuhusu uuzwaji wa hisa za kampuni ya Glencore Canada Corporation na Barrick Gold Corporation wamiliki wa mgodi wa Nickel wa Kabanga mkoani Kagera.

Simbachawene Jumamosi iliyopita aliteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo kuchukua nafasi ya Profesa Sospeter Muhongo.

Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo jana kumkabidhi ofisi Waziri Simbachawene na  kutoa ripoti maalumu ambayo ndani inaeleza mbinu za kuondoa umasikini wa Watanzania kupitia wizara hiyo yenye fursa na rasilimali nyingi.

Profesa Muhongo akimkabidhi ripoti aliyoiandaa kwa wiki moja akisema anamuamini kiutendaji kwani alikuwa naibu wake kwa kipindi cha mwaka mmoja na ni mchapakazi.

Akipokea ripoti hiyo Waziri Simbachawene alisema juhudi zilizoonyeshwa na Profesa Muhongo ni kubwa na nia ya kuondoa umasikini kwa Watanzania aliyoanza nayo ataiendeleza.

 Akuzungumzia uuzwaji wa hisa Waziri Simbachawene alisema moja ya kampuni hiyo imeamua kuuza hisa kutokana na bei kwenye soko la dunia la Nickel kuzorota na kusababisha uendeshaji kuwa mgumu.

“Baada ya kufuatilia bei ya madini ya Nickel kwenye soko la dunia na ushindani wa mitaji adimu kwa bidhaa mbalimbali, kampuni za Glencore Canada Corporation na Barrick Gold Corporation, zimeamua kuanza mchakato wa kuuza hisa kwenye mradi wa ‘Kabanga Nickel” alisema Waziri.

Aidha alisema  una  thamani ya Dola za Marekani zaidi ya millioni 264 (sawa na Shilingi  bilioni 42.24)  na  faida zilizopatikana ni pamoja na kuongeza mashapo (mashimo yanapochimbwa madini)  na kufikia jumla ya tani milioni 58.2 ya Nickel.

Aliwafahamisha kuwa mradi wa Nickel wa Kabanga ulioko wilayani Ngara una wafanyakazi na wakandarasi 55.

Alisema mgodi huo umekuwa ukisaidia jamii inayoizunguka katika masuala mbalimbali  ikiwamo elimu kwa kutoa  mafunzo ya kiufundi mkoani Kilimanjaro pamoja na miradi mingine  ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa  Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Dk. Reginald Mengi,  alimpongeza Simbachawene kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwani inaonyesha kuwa kazi yake ya awali aliifanya  kwa umakini  alipokuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Ufanisi  ndiyo  aliomrudisha katika wizara hiyo.

Dk. Mengi aliipongeza serikali kwa kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika uuzwaji wa hisa za kampuni hiyo ili waweze kufahamu.

Aidha, Dk. Mengi alisema TPSF itashirikiana kwa pamoja na wizara hiyo kuhakikisha ukuaji wa uchumi shirikishi wa wananchi ili kila mmoja anufaike.

“Watanzania wamekuwa wakisikia uchumi umekuwa lakini wanajiuliza uchumi umekuwaje  kwani hawajaona matunda ya kukua kwa uchumi huo, hivyo  tutashirikiana na wizara kwa ukaribu kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi,” alisema  Dk. Mengi.

Post a Comment

أحدث أقدم