LULU NA KISA CHA MAISHA YA MVUNJA KIKOMBE!

SIKU za hivi karibuni imekuwa ikiripotiwa mtafaruku uliopo kati ya staa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mama wa aliyekuwa nyota wa tasnia hiyo, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa.Miongoni mwa mambo yanayozua hali hiyo, kwa mujibu wa mama Kanumba, ni kitendo cha Lulu kumsahau kama ‘mama’ yake na hivyo kukiuka ‘kiapo’ cha awali cha Lulu kumchukulia mama Kanumba katika udugu wa umama.

Staa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Kiapo hiki kiliwekwa siku chache baada ya Lulu kuachiwa kwa dhamana akitoka kwenye Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam alipokuwa akishikiliwa kwa madai ya kumuua Kanumba pasipo kukusudia.Siwezi kurudia hatua kwa hatua ya tukio hilo, wengi wanalifahamu lakini kwa ufupi tu, kifo cha Kanumba kilichotokea Aprili 7, mwaka 2012, nyumbani kwa marehemu huyo, Sinza ya Vatcan, Dar kilidaiwa kusababishwa na ugomvi mkubwa kati yake na Lulu chanzo kikisemekana kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Lulu alikamatwa, akapelekewa Segerea huku akihudhuria kesi kwenye Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam hadi alipoachiwa kwa dhamana Desemba 12, 2012.
MAISHA YAKE NA
MAMA KANUMBA
Ilikuwa baada ya kutoka jela, Lulu na mama yake, Lucresia Karugila ilisemekana walikwenda nyumbani kwa mama wa marehemu Kanumba, Mbezi ya Temboni, Dar kwa lengo la kumuomba radhi mwanamke huyo kwa yote yaliyotokea (ndiyo ubinadamu).Mama Kanumba aliwapokea vizuri, akawasikiliza, akamkubalia Lulu na ombi lake huku akisema yeye anaamini yaliyojiri ni mipango ya Mungu, akatoa la moyoni kwamba, atamchukulia Lulu kama mtoto wake kuanzia siku hiyo. Kwa maana hiyo, Lulu alichukua nafasi ya marehemu Kanumba.
 

MAISHA YALIENDELEA,
AMANI KILA KUKICHA
Tofauti na baadhi ya watu kuamini kwamba, mama Kanumba (kwa namna yoyote ile) asingekubali kumwona Lulu machoni pake maana akimwona anakumbushwa ‘machungu’ ya kifo cha mwanaye lakini ikawa kinyume, Lulu, mama Lulu na mama Kanumba wakawa kitu kimoja. Wakatangaza udugu.
Hata Lulu mwenyewe alibadili staili yake ya maisha, kujirusha kwa sana kwenye klabu za starehe za usiku kukaisha, sasa akawa mtu wa karibu sana na mama Kanumba kama mama yake.Magazeti Pendwa ya Global Publishers yaliripoti ukaribu wa watatu hao kiasi kwamba, ilikuwa raha tupu! Hapa mama Lulu, pale mama Kanumba, kule Lulu mwenyewe.
Ilifika mahali kila mwaka (tangu 2013), kwenye kumbukumbu ya kifo cha Kanumba, Lulu, mama yake na mama Kanumba walikuwa wakishirikiana kwa karibu sana. Walifika kanisani wote, makaburini wote na kuishia kwa shughuli nyingine.

Elizabeth Michael ‘Lulu’ akiwa na mama Kanumba.
MABADILIKO KWA LULU
Hakuna aliyekuwa akijua kwamba Lulu kumbe ameanza kubadilika. Kwamba, hamtafuti mama Kanumba kama zamani kumjulia hali, hamsaidii kama ilivyokuwa awali.Hali hiyo ilitokea kumkera sana mama Kanumba kiasi kwamba, akizungumza na Magazeti Pendwa ya Global Publishers, siku ya kumbukumbu ya kifo cha Kanumba Aprili 7, mwaka huu kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar ambako ndiko alikozikwa marehemu huyo (Lulu hakufika), mama huyo alisema:
“Nasikitika sana namna ambavyo Lulu amekuwa tofauti na maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi katika kuadhimisha kumbukumbu ya Kanumba. Lakini leo kama hivi, hajatokea.
“Pia nasikitishwa kitendo cha kufanya bethidei ya mdogo wake jana (Jumatatu usiku) kule Posta wakati anajua ndiyo usiku ambao Kanumba alifariki dunia.
“Mbaya zaidi, akiulizwa na watu kwa nini sasa hivi hayupo sambamba na mimi kama zamani, anajibu majibu ambayo hayaeleweki. Kumbe maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi yalikuwa ya usaliti.
“Kwa hiyo na mimi sasa nimeamua kubaki peke yangu kama nilivyo, nitaendelea kumuenzi Kanumba mwanangu kwa sababu mimi ndiyo mama yake.”
Lulu alipoulizwa alijibu kuwa kwa sasa anaendelea na maisha yake na mtazamo mpya, alilia kifo cha Kanumba na hawezi kulia tena.

KWA MAANA HIYO SASA
Mtafaruku wa wawili hao unafanana sana na kisa kimoja nilichowahi kusimuliwa na mke wangu, kwamba kuna familia moja ilikuwa ikiishi na baba na mabinti wawili.Baba wa familia alikuwa mkali kupita kawaida. Mara zote kulipotokea kosa kwa watoto hao, mhusika alichapwa sana ili kukanywa. Hali hiyo ilisababisha kuzua hofu miongoni mwao na kumwogopa baba yao katika hali ya uadui.
Siku moja, binti mdogo alivunja kikombe, kwa kujua baba yake ni mkali sana atakuja kupigwa, alianza kulia mwenyewe huku akimsihi dada yake kuliweka moyoni hilo la kikombe kuvunjika.Dada mtu alimwambia ili asije kumsemea kwa baba yake na kuchapwa, afanye kazi mbalimbali ambazo alimpa. Binti hakuwa na jinsi, alifanya kazi hizo kwa moyo mweupe na kweli hakusemewe.
Lakini ikawa kila siku baba yao akiondoka akiacha maagizo ya kazi za kufanya zikiwemo ngumungumu kama kuchota maji, dada mtu alimwamuru mdogo wake kuzifanya huku akimtishia kwamba akigoma atamwambia baba yake kuhusu kikombe.
Binti alianza kubadilika mwonekano kwa sababu ya kufanya kazi ngumu na nyingi peke yake. Lakini mambo yalipomzidia, siku moja alimwambia baba yake ana shida. Baba alimsikiliza, akafunguka mambo yote kuanzia kwenye kuvunja kikombe hadi kufanya kazi zote peke yake. Huwezi amini, baba huyo alimkumbatia binti yake na kumwambia: “Nimekusamehe kuhusu kuvunja kikombe, adhabu uliyopata ni kubwa mwanangu.” Ukawa ndiyo mwisho wa utumwa!
KWA MAMA
KANUMBA NA LULU
Nimekuwa nikiyapima maneno ya mama Kanumba kwa Lulu na kubaini kwamba, kumbe mama huyo alitaka Lulu aishi maisha ya binti aliyevunja kikombe!Kwamba, kwa vile Lulu alikwenda nyumbani kwake na ‘kuungama’ kuhusu yaliyotokea nyuma na yeye kumsamehe na kuchukuliana kama mama na mtoto wake, alitakiwa kuishi hivyo maisha yake yote hadi kifo.
Mama Kanumba alitaka akikohoa, Lulu kafika. Akiwa na kiu ya maji, Lulu huyu hapa! Akihisi maumivu ya kichwa, Lulu katia timu. Kitendo cha Lulu kuamua kufanya mambo yake na kumsahau yeye, imebidi mama huyo apaze sauti kusema! (kama alivyofanya makaburini).
Naamini Lulu aliliona hilo mapema sana na akavumilia kuhakikisha hafanyi kosa ili mama Kanumba asipaze sauti kwa jamii kumsemea, yeye angewahi kujisemea mwenyewe ili asamehewe na kuwa huru!

Post a Comment

أحدث أقدم