SIYO LAZIMA ALIYEKUTOLEA MAHARI AKUOE?

Katika ulimwengu wa sasa ndoa ni kitu cha heshima. Mwanamke kupata mwanaume wa kumuoa ni jambo la faraja lakini pia mwanaume kumpata mke bora ni kitu kinachoongeza furaha katika maisha.Hata hivyo, suala la kuoana si la kukurupuka, ni suala linalotakiwa kuchukua muda ambapo wawili waliotokea kupendana hupata nafasi ya kuchunguzana katika mambo kadha wa kadha. Kabla ya kufikia hatua ya kuoana, ni lazima mtaanza kuwa marafiki wa kawaida. Kipindi hicho unapata fursa ya kumtathmini kujua kama huyo uliyemzimikia ana vigezo vya kuwa wako wa maisha ama laa.
Ukishajiridhisha kwamba uliyenaye ni mtu aliyedhamiria kukuoa na hawezi kuja kukufanya ukajuta, ingieni kwenye hatua ya uchumba na wakati huo penzi lenu halistahili kuwa la siri tena.
Angalizo
Wakati mko kwenye urafiki wa kawaida, usiwafanye wale ambao wanawazunguka kujua wazi kwamba kuna kitu kinaendelea kati yenu.Abaki kuwa rafiki wa kawaida na ndugu pamoja na marafiki zako hawastahili kumjua, hata kama watataka umtambulishe kwao, waambie ni rafiki tu.Baada ya kuingia kwenye uchumba, hapo sasa kila mmoja lazima ajue nyie mko vipi na mna malengo gani.
Mwanamke kuwa
makini na hili
Kama mwanamke utakutana na mwanaume kwa mara ya kwanza, akakueleza kwamba anataka kukuoa, huyo ni msanii.Nasema hivyo kwa kuwa, hakuna suala la ndoa pale wawili wanapokutana kwa mara ya kwanza. Kubaliana naye pale atakapokuambia anakupenda na baada ya hapo anza kumchunguza kama ni muoaji kweli.
Ukivutiwa naye ufanyeje?
Kimsingi unapovutiwa na mtu fulani na ukakubali kuanzisha uhusiano naye, jambo la msingi ni kuwa makini sana na nyendo zake katika maisha yenu ya kila siku. Mchunguze kwa undani, je anafaa kuwa mke ama mume wako?
Isije ikatokea eti kwa sababu mmekuwa wapenzi kwa muda mrefu basi atakapokutamkia kwamba anataka kukuoa basi ukubali tu hata kama umeona kwamba maisha ya ndoa yenu yanaweza kutokuwa ya furaha.
Chui pia wamo
Tunajua kwamba wapo ambao katika urafiki na uchumba watajifanya wanyenyekevu, wapole na wenye mapenzi ya dhati lakini kumbe hamna lolote, ni chui walioficha makucha.
Siyo kila mchumba
lazima akuoe
Unachotakiwa kujua kwenye ulimwengu wa maisha ya kimapenzi ni kwamba, siyo kila mwanaume ambaye ndugu zako na marafiki wanajua ni mchumba wako na ameshakutolea mahari anastahili kukuoa. Unayo nafasi ya kusitisha uchumba endapo umebaini kitu ambacho kinaweza kuja kukuharibia maisha yako, hata kama mahari imetolewa na bado siku chache ndoa ifungwe. Nasema hivyo kwa kuwa, ukishaolewa hasa kwa ndoa hizi za Kikristo huwezi kuja tena kuomba utoke. Ukiingia umeingia.
Ndiyo maana inaelezwa kuwa, ndoa si kitu cha kubahatisha kwa kuwa ukikosea kuchagua mwenza sahihi, umeharibu sehemu kubwa ya maisha yako yaliyobaki hapa duniani.Watoto wa mjini wanasema, bora kukosea kujenga nyumba kuliko kukosea kuchagua mwenza.  Hitimisho
Nyota njema huonekana asubuhi na kikubwa zaidi unatakiwa kuwa na imani na mtu ambaye una mpango wa kuanza naye maisha ya ndoa. Kuwa na imani na yule uliyejaaliwa kuwa naye. Epuka sana kumfikiria tofauti, epuka kuwasikiliza watu. Nasema hivyo kwa kuwa, unaweza kumpata mtu ambaye Mungu kakupangia awe wako wa maisha lakini watu wakakupa maneno mabaya kuhusu yeye na ukaamua kumuacha.
Lakini pia unaweza kupata mchumba, ukawa ‘unamind’ vitu vidogovidogo, matokeo yake kila mchumba unayempata unaona hafai. Weka akilini kwamba hakuna mtu aliyekamilika kwa asilimia 100.

Post a Comment

أحدث أقدم