MTOTO MIAKA 8 AUAWA NA MBWA

INAUMA sana! Aisha Ally mwenye umri wa miaka 8 (pichani), mkazi wa Mtaa wa NSSF, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu  wa Shule ya Msingi ya St. Joseph, Dar, amefariki dunia baada ya kung’atwa na mbwa anayedaiwa kuwa na kichaa, Uwazi lina mkasa wote.
Aisha Ally anayedaiwa kushambuliwa na mbwa.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni nyumbani kwao Mbezi wakati mtoto huyo alipotumwa na mama yake mkubwa kwenda dukani kununua vocha ya simu.Akisimulia tukio zima kwa waandishi wetu, baba mzazi wa marehemu, Ally Ayub alisema:
“Siku ya tukio mwanangu alitumwa na mama yake mkubwa kwenda dukani kumnunulia vocha, sasa wakati anarudi nyumbani njiani alikutana na mbwa huyo akamshambulia kwenye mguu wa kushoto, mkono wa kushoto na mdomoni.
“Mwanangu alijitahidi kupambana naye ili kujiokoa lakini mbwa naye alikuwa na nguvu, akamng’ata sehemu hizo.”
“Baadhi ya watu waliokuwepo dukani waliona, wengine walianza kulia baada ya kumtambua mwanangu, wengine  walikimbilia eneo la tukio kwa lengo la kumwokoa, mmoja wao alimpiga teke yule mbwa akatokomea kusikojulikana.
“Ndipo yule mtu aliyempiga teke mbwa na watu wengine walimleta mwanangu nyumbani akiwa anavuja damu sehemu alizong’atwa. Niliumia sana! Na bado  nikikumbuka naendelea kuumia.”
Mzazi huyo alisema kwamba, kabla ya kumkimbiza hospitali Aisha, alimpaka dawa aina ya spiriti kwa lengo la kumkausha damu.Aliendelea kusema: “Baada ya hapo tulimkimbiza Hospitali ya Muhimbili, tulipokelewa vizuri lakini cha ajabu hata dawa aina ya yuso tuliambiwa tukanunue nje jambo lililotusikitisha sana.
“Shida kubwa ilikuwa ni mtoto wangu atibiwe hivyo jirani yangu aliyenisaidia gari pamoja na kunisindikiza, alikwenda kununua hiyo yuso, akapakwa na kuchomwa sindano moja, akafungwa majeraha kisha tukaambiwa turudi nyumbani na kupangiwa tarehe nyingine ya kurudi.”
Aisha Ally akiwa hoi hospitali.
Akiendelea kusimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa huku machozi yakimtiririka, mzazi huyo alisema:
“Kumbe kiutaratibu mwanangu alipaswa achomwe sindano nyingine baada ya saa 72 kitu ambacho hakikufanyika wala kushauriwa na wataalam wa hospitali hiyo.
“Baada ya kurudi nyumbani tulishauriana na mke wangu kwamba mwanangu akakae kwa shangazi yake Kibamba kutokana na shughuli zetu kutofautiana, hivyo muda wa kukaa na mtoto mgonjwa ulikuwa finyu.”“Siku chache baadaye nikiwa safarini, nilipigiwa simu na mke wangu, akaniambia amepigiwa simu na wifi yake (Salima) na kumwambia kwamba, Aisha anaumwa.
“Alisema alimpeleka hospitali akapimwa na kukutwa ana malaria 2 hivyo alianzishiwa dozi ya dawa ya mseto.
“Siku mbili mbele nikiwa nimerejea kutoka safari, shangazi wa mtoto alinipigia simu na kunifahamsha kwamba Aisha alikuwa anashtukashtuka.
“Kesho yake nilikwenda kumchukua, nikampeleka Muhimbili kwa maana ya kutibiwa. Ilikuwa majira ya saa sita mchana, akalazwa Wadi B, Chumba J, Jengo la Watoto kisha akapewa vidonge vya kutuliza maumivu.”
“Kesho yake saa sita usiku, siku ya Ijumaa hali ya mtoto wangu ilizidi kuwa mbaya, akawekewa dripu lakini hali iliendelea kuwa mbaya, akahamishiwa Chumba I ambako tulikaa naye kwa takriban saa moja tu, akafariki dunia.” Machozi yakamtoka.Marehemu Aisha alizikwa saa 9 alasiri Aprili 27, mwaka huu kwenye Makaburi ya Ngazija yaliyopo Kisutu jijini Dar.

Post a Comment

أحدث أقدم