Mwili wa aliyezikwa hai wafukuliwa
Mwili
wa mkazi wa kitongoji cha Itezi Magharibi katika Halmashauri ya Jiji la
Mbeya, Nyerere Kombwee, aliyezikwa na wananchi wenzake akiwa hai baada
ya kutuhumiwa kuwa mchawi umefukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya
Rufaa Mbeya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Diwani
wa kata ya Itezi, Frank Maemba, alisema viongozi wa kata hiyo kwa
kushirikiana na polisi wamefanikiwa kuufukua mwili wa mtu huyo na
kuupeleka katika Hospitali ya Rufaa Mbeya ili kusubiri taratibu za
kuuzika upya ziweze kufanyika.
Maemba
alisema uongozi pamoja na wanafamilia wamekubaliana kuwa mtu huyo
atazikwa katika kaburi hilo alilofukiwa akiwa hai ambalo awali lilikuwa
limechibwa kwa ajili ya kumzika mtoto wa kaka yake Leonard Kombwee.
Alisema
kwa upande wa mtoto Leonard ambaye alifariki katika mazingira ya
kutatanisha akihusishwa kulogwa na Nyerere Kombwee ambaye naye ni
marehemu, atazikwa katika kaburi jingine ambalo limechibwa katika
makaburi ya ukoo.
Diwani huyo alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi.
Juzi
wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kali wa kitongoji cha Itezi
Magharibi walimzika akiwa hai mkazi mwenzao, Nyerere Kombwee,
wakimtuhumu kuwa ni mchawi. Wananchi hao walichukua uamuzi huo
wakimhusisha na kifo cha mtoto mdogo wake Leonard Kombwee ambacho
kimetokea katika mazingira yenye utata Aprili 27 mwaka huu.
Chanzo:- Mbeya Yetu
Post a Comment