Marehemu Steven Charles Kanumba.
Mzee Charles Kusekwa.
Bi. Flora Mtegoa.
Mohammed Kuyunga na Joseph Shaluwa
HUKU wingu zito likiwa bado limetanda juu ya kifo cha stadi wa filamu
za Kibongo, Steven Charles Kanumba, baba mzazi wa marehemu, Mzee
Charles Kusekwa ameibuka na kueleza mazito aliyoyataja kama ndiyo
yaliyomponza mwanaye, Risasi Mchanganyiko linakujuza.
Akizungumza kwa njia ya simu wikiendi iliyopita kutokea Shinyanga,
Mzee Kusekwa alisema wanaomtuhumu kuhusika na kifo cha mwanaye wanakosea
kwa vile kuna jambo jingine nyuma ya pazia.
MWANZO WA JAMBO LENYEWE
“Ni vigumu kwa mtu ambaye una mtoto
mkubwa unayemtegemea katika maisha halafu ushiriki kumfanyia mambo ya
kishirikina, hilo haliwezekani hata siku moja.
AANZA KUFUNGUKA
Akienda mbali zaidi, mzee huyo alisema tatizo
lilisababishwa na tambiko ambalo yeye aliliita haramu kwa sababu
halikuwahusisha wazee wa kimila wala kufuata taratibu zinazotakiwa.
Alisema, tatizo ni kijana aitwaye Ayubu Mujungu ambaye ni mpwa wake
(mtoto wa dada yake mzee huyo) aliyemchukua marehemu Kanumba na
kumpeleka kwenye kaburi la babu yake kutambika kinyume na utaratibu wa
mila zao.
“Kama ni matatizo ameyasababisha Ayubu ambaye kwa ujeuri tu
alimchukua marehemu na kumpeleka Simiyu kwa ajili ya kutambika katika
makaburi ya wazazi wangu.
“Binafsi miye na wazee wenzangu
tulishangaa kuona kijana huyo akimchukua mtoto mwenziye (Kanumba) na
kwenda naye kutambika katika makaburi bila ya kuwajulisha wazee.
“Kikwetu suala la matambiko hufanywa kwa taratibu maalum tena chini ya
usimamizi wa wazee. Siyo mtu yeyote anaweza kwenda kufanya tambiko,”
alisema.
ALIKIUKA MASHARTI
Alisema jambo jingine linalomfanya ahusishe
tambiko la Kanumba na Ayubu katika kifo hicho ni kitendo cha marehemu
kukiuka masharti ya kufanya tambiko kwa kuvaa mavazi siyo.
“Kuna kosa lingine Kanumba alilifanya, alivaa nguo nyeusi ambazo wazee wanasema kuwa haziruhusiwi kwenda nazo huko,” alisema.
Mzee Kusekwa alisema kuwa matokeo ya kukiuka mavazi, baada ya Ayubu
na Kanumba kufika makaburini walikutana na vitu vya ajabu ambavyo mpaka
leo ni Ayubu tu ndiye anayevijua lakini hataki kuviweka wazi.
Alizidi kuweka wazi kuwa ili kuwafunga midomo watu waliokuwa kwenye eneo
la makaburi na kushuhudia maajabu yaliyowatokea wawili hao, waliwapa
shilingi laki moja ili wasiseme.
“Hicho ndicho kilichosababisha kifo
cha Kanumba kwa kuwa walikwenda kufukia vitu kwenye kaburi. Baada ya
tukio lile mwanangu aliporejea Dar ndiyo akapata matatizo,” alisema.
KUHUSU MALI ZA KANUMBA
Mzee Kusekwa alisema muda wowote wiki hii
atatua jijini Dar es Salaam kufuatilia suala la mali za mwanaye ambazo
anadai amesikia zimeanza kuuzwa kiaina.
“Kuna kesi nimefungua
Mahakama Kuu kuhusu kuzuia mali za mwanangu kuuzwa, hilo ndilo haswa
linalonileta Dar. Kuna watu wanasema eti kwa mila za Kisukuma sistahili
kuwa mrithi kwa sababu sikumtolea mahari mama Kanumba, hao wanakosea
sana.
“Duniani kote watu wameshindwa kufananisha thamani ya fedha na uhai
wa mtu, hakuna anayejua thamani ya mbegu ya Kanumba, hivyo kama
sikumtolea mahari mama yake siyo sababu ya kunizuia kurithi mali za
mwanangu. Mimi ndiye msimamizi wa mirathi,” alisema.
AMCHAMBUA AYUBU
Mzee Kusekwa alisema, chokochoko zote hizo
amezileta Ayubu ambaye ni mtoto mdogo, akasema yeye (Ayubu) hajui mzee
huyo na mama Kanumba walikutana wapi na walioana au hawakuoana.
Ameongeza kuwa Ayubu ni mtu wa kuchunga sana kwa kuwa tayari
ameshajipendekeza kwa mama wa marehemu ili atajwe kama msimamizi wa
mirathi wakati si mtu wa ukoo wao.
AMSHAURI MAMA KANUMBA
Katika kile kilichoonekana kutuliza hali ya
hewa, mzee Kusekwa alitoa maneno aliyosema kuwa ni ushauri kwa mzazi
mwenzake, Flora Mtegoa.
“Namsihi mzazi mwenzangu asisikilize maneno
ya Ayubu maana ni mchonganishi, sisi tulishafanya kikao cha wanandugu
lakini hakutokea, tukamtafuta na polisi kutokana na maneno yake
akajificha uvunguni, bahati mbaya hatukuwa na hati ya kuingia ndani,”
alisema na kuongeza:
“Aache kuamini ushirikina kwa kusema mtoto
amechukuliwa msukule, hakuna msukule hapo ni matatizo ya tambiko.
Kikubwa kwake kwa sasa ni kujenga imani kwa Mungu kwa kuwa ndiye
aliyemchukua kiumbe wake.”
AYUBU KIKAANGONI
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Ayubu kwa njia
ya simu na kuzungumza naye kuhusiana na madai hayo ya mjomba wake ambapo
alitoa ushirikiano wa kutosha.
Kwanza, alianza kwa kukiri
kuongozana na merehemu Kanumba kwenye makaburi yanayozungumziwa, akasema
aliyewaagiza kufanya hivyo ni mama wa staa huyo Bi. Mtegoa.
“Tangu mwaka jana, mama Kanumba aliniagiza nimpeleke ndugu yangu
katika makaburi na siyo kutambika bali ni kwenda kuyafagilia, hivyo
Machi mwaka huu ndiyo tukatimiza,” alisema.
Kuhusu kutokewa na kitu
kibaya makaburini hapo, alikanusha ingawa alikiri kumpatia fedha dada
yake anayemfuata aitwaye Lucy ambaye ni mlemavu wa miguu.
“Hatukuwa tunamhonga, hapana. Yule ni dada yangu, tena anayenifuata
mimi, tuliamua kumpa fedha kwa ajili ya kujikimu. Hata hivyo si laki
moja kama alivyosema mjomba, ilikuwa ni shilingi 80,000.
“Tena nakumbuka mimi nilitoa 50,000 na Kanumba akatoa 30,000 fedha ambazo hazikuwa na sharti lolote lile.”
KUHUSU KANUMBA KUVAA NGUO NYEUSI
“Kanumba alivaa suruali ya
jeans, rangi siikumbuki vizuri lakini haikuwa nyeusi na shati la rangi
ya kaki. Hakuvaa nguo nyeusi kabisa.”
Madai ya mzee Kusekwa kuwa
anajipendekeza ili awe mrithi wa mali za marehemu Kanumba, Ayubu alisema
si ya kweli na kwamba amejijenga vizuri kimaisha na si kutegemea mali
za urithi.
“Nina pikipiki, gari, nyumba na ninaendesha biashara zangu mwenyewe,
sina shida na mali za marehemu. Kwanza nafahamu kuwa mwenye haki ya
kurithi ni mama mzazi wa Kanumba.
“Hata huko kuondolewa katika ukoo
ni watu wachache tu waliokutana kutokana na ushawishi wa baba Kanumba
na sijapewa taarifa yoyote kwa kuwa aliyepangwa kuniambia, Elius Meshack
hajaniambia chochote mpaka sasa.”
Ayubu alisema anashukuru kuwa
yeye amemzika ndugu yake, amemuona kwa mara ya mwisho wakati
alipomvalisha nguo na kumuwekea Biblia katika jeneza lake.
MAMA KANUMBA ANENA YAKE
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa
marehemu amezungumza kuhusu suala la mzazi mwenzake kuharakisha suala la
mali za Kanumba huku akisisitiza ni mapema sana.
Akizungumza kwa
uchungu, nyumbani kwa marehemu Sinza jijini Dar es Salaam wikiendi
iliyopita, mama huyo alisema mzazi mwenzake aache kuzungumzia kuhusu
mali kwa wakati huu kwa vile ni mapema sana.
“Mimi nina uchungu na
mwanangu, lakini mwenzangu naona anajali zaidi mali. Mimi ninalia, bado
nipo kwenye msiba, yeye anasherehekea. Ndiyo maana hakuja msibani, mimi
nimefika kumzika mwanangu, lakini siku chache baadaye, tayari anasema
anazijua mali za marehemu.
“Sina haja na mali za Kanumba, nina nyumba, kazi na mali zangu
nyingine, kwa nini nigombee mali? Nilitamani sana mwanangu anirithi mimi
na siyo mimi nimrithi yeye.
“Ninatambua kuwa yeye ni baba wa
marehemu, hilo halina ubishi, lakini atulie kwanza. Hata arobaini bado
tunazungumzia mali, za nini? Halafu haya mambo yanakwenda kisheria, muda
ukifika tutafungua mirathi mahakamani. Nipo tayari kusimama naye na
siyo kulumbana kwenye magazeti,” alisema Flora.
Akaongeza: “Hata ukiangalia sababu ya kutokuja kumzika mtoto haikuwa
na maana. Mimi nilipopata taarifa mara moja nilifika, lakini mwenzangu
akasubiri kamati ya mazishi impatie utaratibu na nauli. Utawezaje
kusubiri kamati wakati umefiwa na mwanao?
“Kitu cha kushangaza
alitumiwa nauli lakini hakufika kwa visingizio ambavyo mimi naviona
havina maana. Hebu angalia, mfano alisema eti anaumwa, mbona alitumiwa
nauli ya ndege? Usafiri wa ndege una shida gani? Ndiyo maana mimi nasema
wakati mimi maumivu yangu yakiwa kwenye msiba, mwenzangu anawaza kupata
mali, sasa asubiri muda ufike.”
Bi. Flora alikuwa katika sura ya majonzi muda wote, alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu, lakini hali ilibadilika ghafla katikati
ya mahojiano baada ya ndugu zake waliofika kumpa pole nyumbani hapo.
Ni kama msiba ulianza upya, maana alishindwa kujizuia na kuangua kilio, hivyo kusababisha wageni hao kujumuika pamoja kulia.
KALAMU YA MHARIRI
Kanumba amefariki dunia, ameshazikwa. Hakuna wa
kubadili ukweli huu. Ni vyema sasa wazazi wakakutana na kujadiliana
pamoja kuhusu suala la mirathi na kuacha kutupiana lawama. Majadiliano
yenye usawa ni bora zaidi ya malumbano
Chanzo:- http://www.globalpublishers.info


إرسال تعليق