Chadema: Tatizo si mawaziri tu, bali mfumo

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekosoa kusudio la kusuka upya Baraza la Mawaziri unaotarajiwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete muda wowote kuanzia sasa na kusema tatizo linalokabili nchi sasa ni mfumo uliooza kwa maana hiyo mabadiliko hayo hayataleta tija. Kutokana na hali hiyo, wamesema uteuzi huo ni sawa na kubadili mtindo wa kusuka huku msusi akitumia nywele zile zile za zamani. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, wakati akisoma maazimio 16 ya Baraza Kuu la Chama hicho lililokutana juzi.

Mnyika alisema mwaka 2008, Rais Kikwete alivunja Baraza lake la Mawaziri na kuteua watu wengine ambao hata hivyo, hawakuleta mabadiliko huku waliokuwa wanatuhumiwa kwa ufisadi ambao waliachwa wakati huo mpaka sasa hawajachukuliwa hatua hatua zozote za kisheria. Rais Kikwete alilivunja baraza hilo baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuguswa na kashfa ya zabuni ya kufua umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond ya Marekani, ambayo baadaye iligundulikwa kuwa ilikuwa kampuni hewa. Sambamba na Lowassa, mawaziri wengine waliojiuzulu Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Dk. Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki). “Aina ya kusuka inaweza kubadilika, lakini nywele zitakazotumika zikawa zilezile kama mnakumbuka mwaka 2008, Watanzania walitarajia mawaziri waliokuwa wanatuhumiwa wangefikishwa katika vyombo vya sheria na kushtakiwa, lakini mpaka leo bado tunawaona wanatesa mitaani,” alisema Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo.

Alifafanua kuwa uozo ndani ya serikali haupo kwenye Baraza la Mawaziri pekee bali ni mfumo mzima na kwamba unatakiwa kubadilishwa wote ili kuondoa vitendo vya wizi wa mali za umma. Alisema hata kama Rais Kikwete atateua Baraza la Mawaziri hakutakuwa na jipya kwa kuwa atateua wabunge hao hao wa CCM ambayo wengi wao walipatikana kwa njia za kifisadi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mnyika alisema kuna orodha ndefu ya mafisadi iliyowahi kutolewa hadharani na Chadema mwaka 2007, lakini mpaka leo hakuna hatua zozote zilichukuliwa dhidi yao. Aidha, Mnyika alisema Baraza Kuu la Chadema limesema kitendo cha Kamati Kuu (CC) ya CCM, kubariki kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri bila keleza hatua za kuwachukuliwa mawaziri wanaotuhumiwa ni sawa kuendelea kulinda wezi wa mali za umma.

HALI MBAYA YA UCHUMI
Kuhusu hali ya uchumi nchini, Mnyika alisema Baraza Kuu la chama hicho limesikitishwa na kuendelea kupanda kwa gharama za maisha miongoni mwa wananchi sambamba na kuongezeka kiwango cha mfumko wa bei. Alisema hatua hiyo imesababishwa na uongozi dhaifu wa serikali ya CCM, ambayo imeshindwa kudhibiti matumizi ya mabaya ya fedha za serikali na idara zake.

Mnyika alisema Baraza Kuu la Chadema, lilisitiza kuwa hali ngumu ya uchumi inayoikabili nchi ni kutokana na ukaidi wa serikali ya CCM wa kukataa ushauri na mawazo mbadala ya katika kuongoza nchi. Alitoa mfano kuwa mapato ya serikali kwa mwaka ni tilioni 13.4 wakati makusanyo ya serikali ni Sh. tilioni 7.5 hatua ambayo inawafanya wananchi kuwa na matumaini ya maisha bora wakati bajeti waliosomewa bungeni haitekelezeki.

“Hali hii ya maisha inaweza kuwa mbaya kutokana na utawala huu mbaya wa CCM kwa kuwa chama hiki kimeshindwa kubuni na kusimamia sera sahihi katika kulinda rasilimali za taifa yakiwemo madini, gesi asilia, mafuta, misitu, bahari na ardhi,” alisema Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini.

Alisema Baraza Kuu la chama hicho, limewaagiza wabunge wa Chadema kuwahimiza wananchi ili kuishinikiza serikali ya CCM ili kutimiza wajibu wake na kwamba kikwazo kikubwa cha maendeleo ya Tanzania ni CCM ambayo inaendesha serikali kwa mfumo wa rushwa na ufisadi.

Alisema Baraza Kuu la Chadema, limewaagiza wabunge wake wote wa kuendelea kuiwajibisha serikali na kuhakikisha katika bajeti ya serikali ijayo wanapambana ili iwe ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.

MAUAJI YA MAKADA WAKE
Katika hatua nyingine, Chadema kimesema kinapanga kufungua mashitaka binasfi dhidi ya serikali kwa kushindwa kuwalinda raia wake kufuatia vitendo vya mauaji ya makada wa chama chao katika maeneo ya Arusha, Mbeya, Mwanza, Mtwara na maeneo mengine ya nchi.
Chadema kimesema kinataka kundwa chombo huru kwa ajili ya kuchunguza mauaji hayo badala ya utaratibu wa sasa ambapo Jeshi la Polisi linahusika na vitendo halafu linaunda kamati kwa ajili ya kuchunguza.

KATIBA MPYA
Mnyika alisema Baraza Kuu la chama limewaagiza wabunge wake, kuzunguka nchi nzima kufanya operesheni ya kuwaunganisha wananchi kuhusu masuala ya Katiba mpya na uwajibikaji wa serikali.

UCHAGUZI NDANI YA CHAMA
Wakati huo huo, Chadema kimesema mwaka huu kitafanya uchaguzi ndani ya chama kuanzia ngazi ya chini mwaka huu hadi Oktoba mwakani kwa kuchagua viongozi wa kitaifa. Mnyika alisema chama kimeandaa kanuni maalum ili kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo kwa kuwa Chadema kinapinga vitendo hivyo na lazima kiwe mstari wa mbele kuvipinga.

MISHAHARA KWA WAFANYAKAZI
Kuhusu nyongeza za mishahara kwa wafanyakazi, Chadema kinaitaka serikali kuangalia suala hilo ili kuhakikisha watumishi wake wanalipwa vizuri kulingana na hali ya halisi ya maisha ilivyo kwa sasa. Baadhi ya wabunge hivi karibuni walitia saini azimio la kuwasilisha hoja bungeni ili ijadiliwe kwa lengo la kutaka kumung’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ikiwa serikali ingeshindwa kuwawajibisha mawaziri wanane waliotajwa kuhusika na vitendo vya ufisadi kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ripoti za kamati za kudumu za Bunge za Mashirika ya umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).Hatua ya kutaka kumwajibisha Pinda ilitokana na ripoti hizo kuwagusa baadhi ya mawaziri na wabunge kuwataka wajiuzulu, lakini wakakataa.

Miongoni mwa mawaziri waliotajwa katika ripoti hizo ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC). Alitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma. Pia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi. 

Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, naye anadaiwa kushindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika, ambaye anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika. Yupo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anayetuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme na kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.

Pia yumo Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye atauhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi. Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam; Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za mdororo wa uchumi.
NA RICHARD MAKORE
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post