Jiji la Mwanza kuwaondoa wamachinga Makoroboi
Halmashauri
ya Jiji la Mwanza imesema kwamba inakusudia kuwahamisha wafanyabishara
ndogondogo maarufu kama wamachinga wanaopanga na kuuza bidhaa zao katika
eneo la Makoroboi ikiwa ni utekelezaji wa Sheria Ndogo ya Mipango Miji.
Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo, Wilson Kabwe (pichani), amesema kuwa azma ya
kuwaondoa wamachinga hao inatarajiwa kutekelezwa wakati wowote baada ya
taratibu kukamilika.
Alisema
kuwa katika kutenga maeneo rasmi kwa ajili wamachinga kufanyia biashara
zao, Kamati ya Mipango Miji, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri hiyo
iliweka vigezo kwa ajili ya kuepusha muingiliano wa shughuli za kijamii
na biashara.
Kwa
mujibu wa Kabwe, baadhi ya vigezo vilivyowekwa na Kamati hiyo ni kwamba
maeneo yenye nyumba za ibada, shule pamoja na hospitali hayapaswi
kutumiwa na wamachinga kwa biashara zao.
Alibainisha
kuwa eneo la Makoroboi, lina nyumba za ibada za Jumuiya ya Hindu na
Swaminnarayan pamoja na shule ya watoto wadogo na kwamba ni wakati
mwafaka kwa wamachinga kuanza kuhama wenyewe na kwenda maeneo
waliyotengewa rasmi kwa ajili ya biashara zao.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo ni barabara ya Liberty-Uhuru, Relini, Mwananchi, Kamanga, Kitangiri, Kiloleli na Mkuyuni.
Habari na - GEORGE RAMADHAN
SOURCE: NIPASHE
إرسال تعليق