WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, amekanusha taarifa zinazotapakaa kuwa ana mpango wa kuingia
katika kinyang’anyiro cha kugombea urais ifikapo mwaka 2015, akidai hana
hiyo ndoto, na kutaka watu wanaotoa taarifa hizo alizosema ni za uongo
wachukuliwe hatua.
Membe alisema kuwa nafasi hiyo inahitaji mtu makini, asiye kurupuka,
kwani ni ngumu na lazima mtu awe na vigezo ili kukidhi haja ya wananchi.
Membe akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema alitaka ubunge
akiwa na dhamira na ndiyo maana akashinda nafasi hiyo, na wala hafikirii
suala jingine likiwamo la urais.
Aidha, waziri huyo alikanusha taarifa zilizotolewa na mwanasiasa mmoja
aliyedai kuwa amejilimbikizia mali nyingi ikiwamo kuhodhi hoteli.
“Nyinyi waandishi naomba mumtafute mtu huyo ili athibitishe jambo
hilo, anasema nilitakiwa kuondoka katika baraza lililoundwa hivi
karibuni na rais kama kina Ngeleja na Maige, kitu ambacho si sahihi,
kama hanifahamu mpelekeeni picha yangu na jina ili athibitishe hayo,”
alisema Membe.
Kwa muda mrefu sasa, jina la Membe limekuwa miongoni mwa Wana CCM
wanaotajwa kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi ya
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika hatua nyingine, Membe amedai kuwa watu wajanja wamefanikiwa
kuuza kinyemela zaidi ya ekari milioni 14 kwa wageni, hali inayotishia
uwezekano wa kutokea unyang’anyi wa ardhi.
Membe alisema ikiwa viongozi hawatachukua hatua madhubuti kuhakikisha
ardhi kama rasilimali muhimu inalindwa na kuwasaidia kutumika kukuza
uchumi, kutaleta balaa. Badala yake alisema ni sharti sasa bidii
ichukuliwe kuunda uchumi na kuukuza ili kuleta viwanda vitakavyowapatia
vijana ajira.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment