Siutaki urais - Membe


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amekanusha taarifa zinazotapakaa kuwa ana mpango wa kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea urais ifikapo mwaka 2015, akidai hana hiyo ndoto, na kutaka watu wanaotoa taarifa hizo alizosema ni za uongo wachukuliwe hatua.
Membe alisema kuwa nafasi hiyo inahitaji mtu makini, asiye kurupuka, kwani ni ngumu na lazima mtu awe na vigezo ili kukidhi haja ya wananchi.
Membe akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema alitaka ubunge akiwa na dhamira na ndiyo maana akashinda nafasi hiyo, na wala hafikirii suala jingine likiwamo la urais.
Aidha, waziri huyo alikanusha taarifa zilizotolewa na mwanasiasa mmoja aliyedai kuwa amejilimbikizia mali nyingi ikiwamo kuhodhi hoteli.
“Nyinyi waandishi naomba mumtafute mtu huyo ili athibitishe jambo hilo, anasema nilitakiwa kuondoka katika baraza lililoundwa hivi karibuni na rais kama kina Ngeleja na Maige, kitu ambacho si sahihi, kama hanifahamu mpelekeeni picha yangu na jina ili athibitishe hayo,” alisema Membe.
Kwa muda mrefu sasa, jina la Membe limekuwa miongoni mwa Wana CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika hatua nyingine, Membe amedai kuwa watu wajanja wamefanikiwa kuuza kinyemela zaidi ya ekari milioni 14 kwa wageni, hali inayotishia uwezekano wa kutokea unyang’anyi wa ardhi.
Membe alisema ikiwa viongozi hawatachukua hatua madhubuti kuhakikisha ardhi kama rasilimali muhimu inalindwa na kuwasaidia kutumika kukuza uchumi, kutaleta balaa. Badala yake alisema ni sharti sasa bidii ichukuliwe kuunda uchumi na kuukuza ili kuleta viwanda vitakavyowapatia vijana ajira.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz

Post a Comment

أحدث أقدم