Baraza la CWT laitiisha serikali

BARAZA la Chama cha Walimu Nchini (CWT), limetoa siku 30 kabla ya kutangaza mgogoro na serikali kwa madai kuwa imeshindwa kuteua baraza la majadiliano la sekta ya elimu ambalo lingeweza kujadili mishahara mipya ya walimu kwa mwaka 2012/2013 na kufika asilimia 100.
Tamko hilo lilitolewa jana na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, katika mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa ni kutoa maazimio yaliyofikiwa katika kikao cha dharura cha baraza hilo kilichofanyika Juni 5, mwaka huu.
Mukoba alisema katika kikao cha Januari, mwaka huu, baraza hilo pamoja na mambo mengine liliazimia kuwa serikali iwaongezee walimu mishahara kwa asilimia 100, itoe posho kwa asilimia 55 kwa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na asilimia 50 kwa wanaofundisha masomo ya sanaa.
Na pia walimu ambao wanafanya kazi kwenye wilaya zenye mazingira magumu kwa mwezi kiwango chao kiwe ni asilimia 30.
Sambamba na hilo baraza liliagiza uongozi wa juu wa chama kuwasilisha mapendekezo hayo serikalini kwa lengo la kujadiliana na serikali na majadiliano kukamilika kabla ya Aprili mwaka huu ili makubaliano yatakayoafikiwa yataekelezwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2012/2013.
Pamoja na jitihada hizo, Mukoba alidai kuwa serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, imeshindwa kuteua wajumbe wa baraza hilo.
“Kutokana na serikali kutokuwa tayari kujadiliana na CWT kuhusu nyongeza ya mishahara kwa mwaka ujao wa fedha na kwa kuzingatia katiba yetu Baraza la Taifa limeazimia kutangaza mgogoro wa kikazi na serikali,” alisema.
Katika hatua nyingine, CWT imekiri serikali kupunguza deni la sh biloni 52 walizokuwa wanaidai awali hadi kubakia sh bilioni 13 ambazo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, aliahidi kulimalizia ndani ya mwezi huu.

Post a Comment

أحدث أقدم