MAWAKILI wanaomtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania Nchini Italia,
Prof. Costa Mahalu, na Meneja Utawala na Fedha, Grace Martin, wameiomba
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, awaachie huru katika
kesi ya wizi wa euro milioni tatu kwa madai kuwa upande wa jamhuri
umeshindwa kuthibitisha kama walitenda makosa hayo.
Balozi Mahalu aliwasilisha maombi hayo jana mchana kupitia mawakili
wake Mabere Marando, Beatus Malima, Alex Mgongolwa na Cuthbert Tenga kwa
njia ya maandishi kama walivyoamriwa kufanya hiyo na Hakimu Mfawidhi
Ilvin Mugeta.
Kwa mujibu wa maombi hayo, mawakili waliikumbusha mahakama kuwa
washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita likiwemo kosa la kula njama,
za kuiba euro milioni mbili, kughushi vocha za manunuzi ya jengo la
ubalozi, kutumia risiti za manunuzi kuidanganya serikali, kuisababishia
serikali hasara ya euro milioni 3.
Kwa mujibu wa hoja zao tano muhimu ambazo wamezitumia kuwasilisha ombi
hilo, kwanza wanasema serikali ilimruhusu Mahalu kununua jengo la
ubalozi kwa njia ya mikataba miwili kwa bei ya euro 3,098,741.58 na
kwamba alileta vielelezo kadhaa ambavyo viliweza kuithibitishia mahakama
hiyo kuwa serikali iliridhia jengo hilo linunuliwe.
Walisema kuwa hakuna ushahidi wowote ulioletwa na upande wa jamhuri
kuwa washtakiwa walifanya siri na kutenda kosa la wizi na katika hoja ya
pili walisema kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi
unaoonyesha muuzaji wa jengo hilo kuwa hakupokea fedha hizo euro milioni
3.
Katika hoja yao ya tatu, mawakili walisema ripoti tatu za thamani ya
majengo zilizoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, muuzaji na ubalozi wa
Tanzania nchini Rome hazikuandika jengo hilo lilikuwa na thamani ya
chini ya euro milioni 3.
Ripoti zote ziliandika jengo hilo lilikuwa na thamani ya zaidi ya euro
milioni tatu na kwamba upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi
unaoonyesha wakati huo jengo linanunuliwa lilikuwa na thamani ya kiasi
gani na kwa maana hiyo jamhuri ilikuwa haifahamu thamani ya jengo hilo
wakati serikali inalinunua.
“Hoja ya tano sisi tunadai kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuleta
ushahidi ambao ungeonyesha nani ni mmiliki wa akaunti mbili ambamo euro
milioni 3 zilitumwa na ubalozi wa Tanzania nchini Rome.
Kwa hoja hizo tano tulizozitaja hapo juu, tunaiomba mahakama hii
iwaone washtakiwa hawana hatia kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa
kuleta ushahidi ambao utaishawishi mahakama iwatie hatiani,” alidai
wakili Marando.
Mahakama hiyo inatarajia kutoa hukumu yake Julai 11 kwa kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2007.
Chanzo:- Tanzania Daima
إرسال تعليق