CHADEMA kuwakataa viongozi wa CCM
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza rasmi
kusitisha kuwapokea viongozi wa ngazi zote watakaohama kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na vyama vingine, baada ya kutemwa katika kura za maoni
kwa lengo la kutaka kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alitoa msimamo huo jana
alipokutana na wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya Udom, CBE na St John,
katika hafla ya kuwaaga wenzao wanaomaliza masomo yao.
Mbowe alisema kuwa, CHADEMA kinataka sasa kupata viongozi na wanachama
wanaosukumwa na uzalendo wa kweli, na wanaoamini itikadi na sera zake,
na si wanaotaka kukitumia kama ngazi ya kufanikisha malengo yao.
Alisema wamejifunza kwa kiasi kikubwa hasara ya kuwapokea wanachama,
na hasa waliokuwa viongozi wa vyama vingine dakika za mwisho, hususan
wakati wa uchaguzi, hivyo kuanzia sasa hawapo tayari kufanya hivyo.
Mbowe alisema wapo tayari na wanawakaribisha wanachama ama viongozi wa
CCM ambao wanaona kuwa CHADEMA ni chama makini, kikomavu na wanaoamini
kina malengo halisi ya kuikomboa nchi na kuwaletea maendeleo wananchi
wote bila kujali itikadi ya vyama, dini, kabila ama eneo la nchi.
“Wale wapambanaji waliochoshwa na matendo ya wenzao ndani ya CCM, na
wanaoamini kwa dhati kabisa na kusukumwa na dhamiri ya kweli ya
kupigania maslahi ya wanyonge, waje sasa.
“Hakuna haja ya wao kusubiri hadi dakika za mwisho, na hasa pale
wanapopigwa chini katika kura za maoni ndio waje. Wajue kuwa wakisubiri
muda huo, hawataweza kupokelewa hata kama watakuwa ni wazuri namna
gani,” alisema Mbowe.
Kuhusu vitisho
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro alisema kuwa
serikali baada ya kuona kuwa inaelemewa, imeamua kuwatisha na kuwafukuza
wanachama wa CHADEMA katika vyuo na sehemu za kazi, kama njia ya
kudhibiti kasi ya chama hicho.
Alisema kuwa amepata taarifa za kuaminika, kutoka sehemu mbalimbali
nchini, kwamba baadhi ya wanavyuo wamekuwa wakitishwa na hata kufukuzwa
kwa tuhuma za kubambika kwa kile alichodai ni mbinu za kujaribu
kudhohofisha nguvu za upinzani bungeni.
Mwenyekiti huyo, alisema kuwa mtindo wa kutisha na kufukuza watu hauko
katika vyuo tu, bali umeingia hata serikalini, na sehemu zingine.
“Serikali ya CCM sasa imeamua kutumia mbinu chafu kukandamiza haki za
watu baada ya kuona kuwa sasa tumewaamsha kutambua haki zao. Wamebuni na
kutambua kuwa wakiwafukuza wanavyuo wazazi watakasirika na hivyo kuona
kuwa CHADEMA ni hatari,” alisema.
Aliwataka wanavyuo hao kusimama imara na kuonesha msimamo wao na
kueneza elimu ya uraia na ilani ya CHADEMA, bila kuwabeza wala
kuwakashifu viongozi wa kisiasa waliopo katika maeneo ya vijijini hata
kama ni wa CCM.

إرسال تعليق