Kim aachwe afanye kazi - Mogella

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Taifa Stars na Simba, Zamoyoni Mogella amesema tatizo linaloisumbua timu ya taifa, Taifa Stars ni 'kuwekewa mikono mingi' na wanaojifanya watu wa wa ufundi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.

Mogella aliyepachikwa jina la 'Golden boy' kwa umahiri wa kufumania nyavu, alisema endapo viongozi wa TFF na wanaojiita Kamati ya Ufundi wakikaa pembeni na kumwacha Kim Poulsen akafanye kazi yake, timu itafika mbali.

"Sitaki kuizungumzia Twiga Stars timu isiyoangaliwa kwa kuwa haina maslahi kwa viongozi huku ikiwa chini ya kocha ambaye alipewa Kilimanjaro Stars kwenye Chalenji akaharibu, ukweli ni kwamba Kim yupo makini naamini timu itasonga mbele kwa kuwa ana wachezaji makini.

"Tatizo liko kwa viongozi, wapo kama hawapo wanaangalia maslahi yao zaidi lakini mwalimu angeachiwa timu afanye kila kitu hasa masuala ya ufundi na kupata anachokitaka katika timu imeonyesha uwezo mkubwa tangu iwe mikononi mwa Kim," alimalizia Mogella.

Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga, Bakili Makele alisema Taifa Stars inahitaji muda kwa kuwa ina vijana wengi ambao wanahitaji kupata uzoefu zaidi.

"Timu ni nzuri ipewe muda wa kujipanga itafanya vizuri zaidi lakini pia TFF ikubali maombi ya mwalimu kuanzia mazoezi endelevu kwa kila nafasi inapopatikana," alisema Makele.

Katika hatua nyingine, wadau wa soka jijini Dar es Salaam wamelitupia lawama Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuwa ndio chanzo cha kufanya vibaya Twiga Stars kutokana na kuwa na wachezaji wale wale kila siku.

Sufiani Rajabu mmoja wa wapenzi wa soka, alisema inahitaji kuundwa upya ikiwemo kupata wachezaji watakaoipa nguvu timu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Naye Isaack Togocho, mwenyekiti wa Chama cha Pool Taifa, alishauri TFF alisema viongozi wa TFF wanaiona timu inapokuwa na majukumu ya mechi za kimataifa na kuisahau inapomaliza mashindano kitu kinachovunja nguvu wachezaji na viongozi

Post a Comment

Previous Post Next Post