Sasa watuhumiwa kupoteza bil. 300/-
MAWAZIRI wawili wa zamani katika Wizara ya Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige na Shamsha Mwangunga, wanatuhumiwa kuliingizia taifa hasara ya sh bilioni 300, kwa kutumia madaraka yao vibaya.
Tuhuma hizo nzito zimetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe, ambaye
alidai hasara hiyo kubwa imetokana na uzembe uliofanywa na mawaziri hao
wa zamani wakati wakiiongoza wizara hiyo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara
baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo na watendaji wakuu wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) Filikunjombe ambaye ni mbunge wa
Ludewa (CCM) alisema kuwa Mwangunga ambaye alikuwa waziri, huku Naibu
wake akiwa ni Maige, waliizuia mamlaka hiyo kutoza tozo zinazotolewa
katika hoteli za kitalii kwa muda wote waliokuwa madarakani.
Alisema uzembe huo umeathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa serikali na
iwapo shughuli hiyo ingeachiwa hifadhi hiyo ya taifa kwa mwaka
wangeweza kukusanya kiasi cha sh bilioni 21.
“Pamoja na kuwa taarifa yao ni nzuri lakini sisi kama kamati
tumegundua uzembe uliofanywa na Mwangunga pamoja na Maige juu ya jambo
hilo maana fedha hizo zingeweza kujenga barabara na shule kila maeneo,”
alifafanua.
Alisema matatizo mbalimbali yanayolikabili taifa hili yanachangiwa kwa
kiasi kikubwa na wanasiasa hivyo aliwataka kuacha shughuli za mashirika
kufanywa na bodi walizonazo.
“Matatizo mengi yanayojitokeza ni kutokana na wanasiasa kuingilia moja
kwa moja shughuli zinazofanywa na mashirika kama ambavyo tumeliona hili
lililowapata TANAPA ambapo kuna maamuzi ya kisiasa yaliyofanywa na
Mwangunga pamoja na Maige,” alisema.
Alisema kipindi cha uwaziri wa Maige alishindwa kulipatia ufumbuzi
suala hilo kwani alilichochea hatua iliyohamasisha waliokuwa wakipinga
uamuzi huo kukimbilia mahakamani.
Alisema hadi sasa TANAPA imepata kiasi cha sh bilioni 4 pekee katika
tozo za hotel hizo zilizo katika hifadhi mbalimbali nchini, hivyo kamati
imeazimia kukutana na wizara hiyo ili kuangalia namna ya
kulishughulikia tatizo hilo.
Machi 21, 2011 wizara hiyo ilitetea sakata hilo la tozo huku
ikimkingia kifua aliyekuwa Waziri Ezekil Maige kuwa hausiki na jambo
hilo.
Katika taarifa hiyo ambayo ilitolewa na msemaji wa Wizara hiyo George
Matiko, ilieleza kuwa mtangulizi wa Maige katika wizara hiyo Shamsa
Mwangunga, ndiye aliyekubaliana na pingamizi la wadau ambao
hawakukubaliana na ongezeko hilo na kuliagiza shirika la hifadhi za
taifa (Tanapa) kusitisha utekelezaji wa tozo mpya.
Alisema Tanapa katika mwaka wa fedha 2008/09 lilipendekeza kuongezwa
kwa tozo za watalii wanaolala katika hoteli na kambi za wageni ndani ya
hifadhi za taifa na kwamba ongezeko hilo lilifuatia vikao vya pamoja
kati ya shirika hilo na wadau mbalimbali katika sekta husika na wengi
wao walikubaliana na ongezeko hilo.
Kwa mujibu wa Matiko, wadau wachache katika sekta hiyo ya hoteli
hawakuridhika na uamuzi huo wa kuongeza tozo hilo na waliamua kupeleka
suala hilo wizarani wakitaka kusitishwa kwa uamuzi huo wakidai kuwa
utaathiri biashara zao.
Kuibuka kwa tuhuma hizo kumezidi kuwaweka waliokuwa mawaziri wa wizara
hiyo katika wakati mgumu wa kujinasua na sakata nzito zinazojitokeza
kila siku.
Kamati za Bunge zacharuka
Katika vikao vyake, Kamati mbalimbali za Bunge zimecharuka na
kuchukua maamuzi mazito yakiwemo ya kuwatimua watendaji wa halmashauri
kadhaa baada ya kutoridhishwa na ripoti za utendaji kazi.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) imekataa kupitia na
kukagua hesabu za halmashauri za Rufiji na Mafia na kulazimika kuwatoa
nje kutokana na kushindwa kuwasilisha taarifa za hesabu zao kwa wakati
mbele ya kamati hiyo.
Licha ya kuwatoa nje pia wajumbe wa kamati hiyo wamewataka wakurugenzi
na wakuu wa idara wa halmashauri hizo kukatwa asilimia 15 ya mishahara
yao kwa mwezi Juni ikiwa ni adhabu kutokana na uzembe huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustino Mrema, alisema wajumbe wa LAAC
wametoa wiki mbili kwa halmashauri hizo kurekebishe hesabu zao na
kuziwasilisha mbele ya kamati hiyo pamoja na Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mrema ambaye ni mbunge wa jimbo la Vunjo (TLP) alisema kamati yake
inadhamiria kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha watendaji
wazembe na wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na mali za umma.
Alisema operesheni ya kusafisha nchi na kuwaondoa mafisadi wanaofuja
fedha na mali za umma ni zoezi endelevu kwa halmashairi zote nchini.
Mwenyekiti huyo hakusita kutoa onyo kali na kutangaza vita kwa
wakurugenzi wa halmashauri nchini ambao wanajihusisha na ufujaji wa
fedha za umma huku wakipuuza maagizo yanayotolewa na kamati yake na kuwa
hawatasita kuwawajibisha.
“Tuliamua kuwatoa nje ya mkutano na kukataa kupitia hesabu zao
kutokana na kuchelewa kuwasilisha vitabu vyao mbele ya kamati...vitendo
vya aina hiyo vinaonyesha kudharau maagizo ya Bunge,” alisema.
Michango ya mafuriko yaibiwa
Nayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeagiza serikali
kuwalipa fidia wananchi wa Mabwepande walioporwa viwanja na kupewa
wahanga wa mafuriko.
Aidha kamati hiyo, imebaini upotevu wa vifaa vilivyotolewa kwa ajili
ya kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana
ambao wamehamishiwa katika eneo la Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar
es Salaam.
Akizungumza jana mara baada ya kutoka kutembelea waathirika hao,
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Zainabu Vullu (CCM), alisema wajumbe wa kamati
hiyo wamebaini upotevu wa mabati 40, saruji mifuko 44, nguo na
magodoro.
“Kuna mifuko 1,500 ya saruji ikiwa inaanza kuharibika bila ya kutumika
kwa matumizi yaliyokusudiwa hivyo tumeagiza wahusika kufanya uhakiki
‘stock checking’,” alisema.
Kutokana na hali hiyo kamati imeipa wiki mbili Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kitengo cha Maafa, itoe maelezo ya upotevu wa vitu hivyo mbele ya kamati
hiyo bungeni mjini Dodoma.
Nayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imewabana
Watendaji wa Mkoa wa Kagera kwa kuidhinisha sh bilioni 4.5
katika mradi wa ujezi wa gati katika ziwa ambao mradi huo
hauendani na fedha hiyo.
Kutokana na madudu ya mkoa wa Kagera imemwita aliyekuwa Katibu
Tawala Maria Bilia ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuidhinisha mradi ambao
hauwezi kutekelezeka kutokana na bajeti kuwa finyu.
Wabunge wamelalamikia mradi wa bilioni 4.5 kuwa ni mkubwa ambao
hadi hatua ya mwisho wametumia sh bilioni 1.5 kwa ujenzi ambao
hauendani na thamani ya fedha.
Akizungumza jana Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alisema
kuwa matumizi ya serikali kwa mkoa huo ni mabaya, na akataja
matumizi ya fedha za ujenzi wa gati kwenda kujenga majengo ambayo
hayakuwa kipaumbele.
Cheyo alisema kuwa mkoa huo umepata hati yenye mashaka katika
miaka miwili mfululizo kutokana na kutumia fedha ya wanyonge katika
miradi mikubwa ambayo inatumia fedha nyingi lakini haishi.
Chanzo:- Tanzania daima (http://www.freemedia.co.tz )
إرسال تعليق