Dk. Bilal akerwa na vurugu Z’bar

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal amesema haoni sababu yoyote kwa watu wanaohubiri kuwa hawataki Muungano kukimbilia kuchoma makanisa na kuvunja baa.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya vurugu za Zanzibar na waandishi wa habari, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa watu saba kutoka Marekani ulioongozwa na Seneta kutoka Delaware, Christopher Coons.
Alisema kuwa, kikundi cha watu hao kimekuwepo siku nyingi na kinatumia kivuli cha dini katika kufanya siasa.
Makamu wa Rais alieleza kuwa, Zanzibar ni kisiwa kidogo na kupitia Muungano wananchi wananufaika na kamwe serikali ya awamu ya nne haiwezi kuvumilia kuona watu wachache wenye agenda iliyojificha wakiharibu jambo bora lililofanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 48.
“Kila ukipita mikoani unakutana na Wazanzibar wanaishi, kupitia Muungano tumefungua fursa nyingi. Sioni sababu ya watu kuibuka sasa kuupinga, na tena kwa kufanya fujo. Tutaendelea kudhibiti hali hii na kuhakikisha kuwa amani inabakia katika nchi yetu,” alisema Dk. Bilal.
Katika mazungumzo yake na ujumbe huo wa Marekani, Dk. Bilali alielezea kufurahishwa kwake na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na pia akafafanua kuwa taifa hilo limekuwa ni rafiki wa kweli kwa Tanzania kutokana na michango yake ya maendeleo iliyopo nchini.
Alisema Serikali ya Tanzania inaona faraja kushirikiana na Marekani na kueleza kuwa mchango wake kwa Tanzania ni mkubwa na hivyo inawataka kujenga ushirikiano zaidi katika sekta za kilimo na nishati.
“Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton alikuja hapa, akatupa matumaini ya kuondokana na tatizo la umeme. Tayari wapo wawekezaji wengi kutoka Marekani ambao wana nia ya kuwekeza katika nishati,” alisema Dk. Bilal.
Hata hivyo, Makamu wa Rais alisema pamoja na juhudi zote za kuhifadhi mazingira na viumbe hai, bado Tanzania inakabiliwa na matatizo ya ujangiri, uvuvi haramu, na magugu maji kufunika kabisa baadhi ya maziwa na mito.
Naye Seneta Coons alisema katika jimbo lake la Delaware wapo wakulima wengi ambao wangependa kuja nchini kuwekeza katika kilimo, huku akieleza Tanzania inavyoweza kuzalisha umeme wa ‘Geothermal’ kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Marekani.

Post a Comment

أحدث أقدم