MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza vita na Mbunge wa Jimbo la Newala,
John Mkuchika kwa kile alichodai ufisadi mkubwa anaowafanyia wakulima wa
zao la korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mbowe akihutubia katika mikutano aliyofanya katika Kijiji cha
Nanguruwe na Viwanja vya Mahakama vilivyopo Newala mjini, alisema
atambana mbunge huyo pamoja na viongozi wengine wakati wa vikao vya
Bunge katika mambo makuu matatu, ikiwemo Jeshi la Polisi, zao la korosho
na ukusanyaji wa mapato.
Alisema Mkuchika ameshindwa kuwasaidia wananchi sambamba na umasikini
mkubwa wanaokumbana nao katika jimbo lake, hivyo atahitaji majibu ya
kueleweka, huku akiwata wasiwe na huruma tena kwa kuendelea kuikumbatia
CCM, kwani imeshindwa kuwasaidia miaka mingi sasa.
Mbowe alisema licha ya jimbo hilo kuwa na utajiri mkubwa na uwezo wa
kilimo cha korosho, mbunge huyo amewatenga, huku serikali yake
ikichekelea kwa kuwatengenezea wananchi mfumo mbaya wa stakabadhi
ghalani, ambao asilimia kubwa ni unyonyaji.
“Nawaambia ndugu zangu wa Newala, safari hii Waziri Mkuu Pinda na
Mkuchika, lazima watanyooka tu, kwani tutawasha moto juu ya matatizo
makubwa ya Lindi na Mtwara kwenye masuala ya upatikanaji wa madini ya
gesi, mafuta, umasikini na juu ya mambo ya kilimo ikiwemo kuwateteeni
juu ya zao la korosho,” alisema Mbowe.
Akemea siasa za dini
Mbowe pia aliwaasa wananchi wa Newala, kuepuka kugawanyika kwa
misingi ya dini, kabila na utabaka ili kuliepusha taifa kuingia katika
vita.
Alisema Serikali ya CCM imekuwa chanzo kikubwa katika kuchochea udini,
kiasi cha kusababisha machafuko ya Zanzibar, kwa kuwaachia baadhi ya
watu kufanya mihadhara ya kichochezi bila kuchukua hatua.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق