KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameahidi
kuwakaba koo mawaziri wawili wa serikali ya Jakaya Kikwete katika Bunge
la bajeti linalotarajiwa kuanza Juni 12 mwaka huu kwa kushindwa kutatua
kero zinazowakabili Watanzania wakati uwezo huo wanao.
Mawaziri watakaokumbana na kibano cha Mbowe ni Bernad Membe, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Hawa Ghasia, Waziri Tawala
za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mbowe aliahidi kuwabana mawaziri hao juzi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kata ya Makanga wilayani Nanyumbu na kuhudhuriwa na
maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo ambao walitoa kero mbalimbali
zinazowakabili.
Miongoni mwa kero hizo ni pamoja na kunyanyaswa pindi wanapotumia
daraja la umoja kati ya Tanzania na Msumbiji kwa ajili ya kwenda nchi
jirani ya Msumbiji hata kama wana vibali vya kuingia nchini humo.
Akielezea namna daraja hilo lisivyowanufaisha Watanzania na badala
yake kuishia kunyanyaswa, Mkazi wa Makanga, Mkapura Omar, alisema
tatizo hilo lilishamkuta yeye pamoja na Watanzania wengine ambao mpaka
leo wako nchini Msumbiji kwa kushindwa kurudi baada ya kunyang’anywa
kila kitu walichokuwa nacho ikiwamo vibali vya kuwaruhusu kuingia nchini
humo.
Tunaomba mtusaidie; tunaonewa sana tunapotumia daraja la Umoja kwenda
Msumbiji, mimi nilikwenda kuwasalimia ndugu zangu; nikafuata taratibu
zote lakini nilipofika nikanyang’anywa kila kitu na askari wa Msumbiji
licha ya kuwa na vibali halali vya kuingia katika nchi hiyo,” alisema
Omary.
Akielezea hali hiyo Mbowe alisema hayo ni matokeo ya sera mbovu ya
mahusiano ya kimataifa zinazowafanya Watanzania kunyanyaswa wanapokuwa
mipakani.
Kuhusu viongozi wa serikali za mitaa wakiwamo madiwani na wenyeviti wa
vijiji kutofanya mikutano na kuwasomea wananchi kile walichokitekeleza,
Mbowe alisema kisheria wanawajibika kufanya hivyo kila baada ya miezi
mitatu na
atamhoji waziri Ghasia ili kujua hatua alizokwishachukua
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz

إرسال تعليق