KOCHA Marcio Maximo wa Brazil aliyekuwa awasili jana kwa mazungumzo
ya kuinoa timu ya Yanga, ameshindwa kufanya hivyo kutokana na timu yake
ya Democrata F.C ya Mjini Rio de Jeneiro, kukabiliwa na mechi muhimu.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, mechi hiyo muhimu
itachezwa Jumamosi hii, hivyo ujio wa Maximo utakuwa baada ya kupita
kwa mechi hiyo muhimu kwa timu hiyo.
“Yanga inapenda kuwajulisha juu ya ujio wa Kocha Marcio Maximo,
aliyetarajiwa kuwasili leo (jana), sasa anatarajiwa kuwasili mwishoni
mwa wiki hii.
“Maximo ambaye tayari amekwishatumiwa tiketi ya safari ya kuja,
ameshindwa kuwasili leo (jana), kutokana na timu yake ya Democrata F.C
ya mjini Rio de Janeiro, Brazil kukabiliwa na mechi ngumu Jumamosi ya
wiki hii,” alisema.
Sendeu alisema, baada ya kuwasili nchini atafanya mazungumzo na
uongozi wa Yanga, ikiwamo kusaini mkataba wa kuinoa timu hiyo kwa
michuano ya
Kombe la Kagame itakayofanyika mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Sendeu, Maximo amewaahidi makubwa wapenzi na mashabiki
wa Yanga kwani baada ya kubeba jukumu hilo, atafanya jitihada za kukiimarisha
kikosi cha ushindi ikiwamo kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame.
Kwa sasa timu yake ya Democrata FC inashiriki michuano maalumu ya majimbo
ikilenga kusaka nyota wa kuichezea timu ya taifa ya Brazil, wenyeji wa fainali za
Kombe la Dunia mwaka 2014.
Sendeu alisema kati ya mambo yatakayopewa msisitizo mkubwa na Maximo
ni uwekezaji kwenye soka ya vijana kwa lengo la kupata nyota wa kesho,
pia
kuimarisha nidhamu kwa wachezaji.
Baada ya kusaini mkataba wa kuinoa Yanga, mtihani wa kwanza kwake utakuwa
kuiwezesha kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame ambalo timu hiyo ililitwaa
Julai 10, mwaka jana chini ya Kocha Sam Timbe wa Uganda.
Michuano ya Kombe la Kagame itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai
23 hadi Agosti 5 ambapo Tanzania Bara itawakilishwa na timu tatu; Simba,
Azam na Yanga.
Ujio wa Maximo unangojewa kwa hamu na wapenzi na mashabiki wa Yanga,
wakiami miaka minne ambayo kocha huyo aliyoishi nchini akiinoa timu ya soka
ya Tanzania, Taifa Stars kati ya 2006 hadi 2010, kutamsaidia akiwa Jangwani.
إرسال تعليق