Polisi yafuta maandamano ya Waislamu
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limepiga
marufuku maandamano ya Waislamu yenye lengo la kupinga Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta) kwa madai kuwa limewafelisha wanafunzi wa dini
hiyo katika somo la elimu ya Uislamu.
Kaimu Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Ahmed Msangi, alisema sababu
za kusitisha maandamano hayo ni kutokana na jeshi hilo kutokuwa na idadi
ya askari wa kutosha kutoa ulinzi kwa vile waumini hao watakuwa
wakitokea katika misikiti mbalimbali.
Alisema kuwa waandamanaji walikuwa na lengo la kwenda katika Ofisi ya
Wizara ya Elimu na Necta lakini tayari kamati ya maandalizi ilikutana
na Waziri wa Elimu Dk. Shukuru Kawambwa pamoja na viongozi wengine
wakafikia muafaka.
Wakati huohuo, Waziri Kawambwa, amewasihi waumini hao kusitisha maandamano kwa vile suala hilo amelishalitolea ufumbuzi.
“Nawasihi jamii, dini na Watanzania wajiepushe na maandamano kwani
maelezo yameshatolewa kwa kina na viongozi wa pande zote
zishakubaliana,” alisema.
Kwa mujibu wa Kawambwa dosari katika somo hilo, imetokana na kutumiwa
kwa teknolojia mpya ambayo imekuwa ni mara ya kwanza kutumika katika
masomo; teknolojia hiyo ilisababisha hitilafu kwa baadhi ya masomo
ikiwemo la Kiislamu, kwani katika masomo yenye karatasi mbili ilitumika
kwa usahihi wakati somo lenye zaidi ya karatasi hizo ilionyesha dosari.
Kawambwa aliongeza kuwa wizara itaunda kamati ya wataalumu kuiwezesha
serikali kujiridhisha zaidi na hatua zilizochukuliwa na Necta ili dosari
hiyo isijirudie.
إرسال تعليق