UINGEREZA YATOA SOMO LA UPIGAJI MBIZI NA UOKOZI KWA KIKOSI CHA KMKM ZANZIBAR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mkurugenzi wa Kampuni zinayotowa Mafunzo ya Uzamiaji na Uokozi za Nchini Uingereza. Mazungumzo yao yalifanyika nyumbani kwa Balozi Seif Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Kampuni zinazotowa mafunzo ya upigaji mbizi na Uokozi { L&W na In Deep Diver Training } za Nchini Uingereza Bw. Jim Kellett akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi nyumbani kwake mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Bw. Jim na Timu yake yuko Nchini kuendesha mafunzo ya Wiki mbili ya uzamiaji na uokozi kwa  Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM.
Mabingwa wa Kampuni inayojishughulisha na masuala ya Mafunzo ya upigaji mbizi na Uokozi ya Nchini Uingereza { In Deep Diver Training } na kampuni ya L&W inakusudia kuendeleza mafunzo ya uzamiaji  kwa Vijana wa Taasisi tofauti za Zanzibar baadaye Mwezi wa Novemba mwaka huu wa 2012.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hizo Bw. Jim Kellett amesema mafunzo hayo yatawashirikisha Vijana 30 kutoka Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, Shirika la Uvuvi wakiwemo pia wawakilishi wa Taasisi za Utalii.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Mafunzo na Huduma za upigaji mbizi alifahamisha kwamba Taasisi yake imeamua kuendesha Mafunzo kama  hayo katika Nchi mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo Vijana wa kutumia Vipaji vyao katika Biashara ya upigaji mbizi.
Amesema mbali ya fani hiyo kutumiwa katika masuala ya uokozi lakini pia itasaidia kutoa ajira kwa Vijana waliomo ndani ya Sekta ya Utalii.
Bw. Jim ameelezea kufurahishwa kwake na mazingira  mazuri aliyoyashuhudia Zanzibar katika nyanja ya uzamiaji.
Aidha ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzipitia Sheria na Kanuni za Uokozi kwa lengo la kuzifanyia marekebisho ili ziende na wakati wa sasa.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza uongozi wa Kampuni zote mbili chini ya Mkurugenzi wao kwa uamuzi wao wa kutoa Mafunzo ya Wiki mbili kwa Askari 30  wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar { KMKM }.

Post a Comment

أحدث أقدم