WAKUU WA SADC WAITAKA ZIMBABWE IWEKE MAMBO SAWA
WAKUU wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao
wamemaliza kikao chao cha siku moja na wamekubaliana kwa pamoja kwamba Serikali
ya Zimbabwe haina budi kukamilisha utaratibu wa kuanzisha mchakato wa Katiba.
Uamuzi huo umefikiwa jana usiku
(Ijumaa, Juni Mosi, 2012) mara baada ya Wakuu wa nchi saba za SADC na
wawakilishi wa nchi saba kuhitimisha kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Talatona
(CCTA), jijini Luanda, Angola.
Katika taarifa yao ya pamoja (joint
communiqué), wakuu hao wameitaka Serikali ya Zimbabwe kukamilisha mchakato wa
Katiba na kisha kuitisha kura ya maoni kama ambavyo ilikubaliwa kwenye Global Political Agreement (GPA) ya
SADC.
“Kikao hiki kinawataka wajumbe wa GPA
wakisaidiwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye pia ni mratibu wa
upatikanaji wa muafaka wa kisiasa Zimbabwe (Zimbabwe Political Dialogue) waweke
mkakati wa utekelezaji wa makubaliano ya GPA utakaoainisha muda wa utekelezaji
wa makubaliano hayo kuelekea uchaguzi mkuu,” ilisema sehemu ya taarifa yao.
Kikao hicho pia kiliridhia kupitishwa
kwa jina la Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma
kuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Mapema mwaka huu, uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo inayoshikiliwa na Bw. Jean
Ping ulishindwa kufanyika kwa sababu kadhaa.
“Kikao hiki kinaipongeza Seriklai ya
Malawi kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa
Afrika ambao umepangwa kufanyika Lilongwe, Julai, mwaka huu. Kwa hiyo basi,
kikao hiki kinataka uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni ya AU ufanyike wakati wa
mkutano huo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika
kikao hicho ni pamoja na hali za kisiasa katika nchi za Congo (DRC), Madagascar
na Malawi.
Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa
SADC, Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola alisisitiza umuhimu wa nchi
wanachama kuweka juhudi za makusudi katika kuimarisha miundombinu kwenye kanda
hiyo ya kusini mwa Afrika.
“Tunapaswa kushirikiana kuimarisha
miundombinu kwenye kanda yetu ya SADC, tukifanikiwa katika hili tutakuwa
tumeweka msingi mkuu wa utangamano wa kikanda, tutaweza kusumuma ajenda ya
kuleta maendeleo na kupunguza umaskini miongoni mwa nchi wanachama,” alisema.
Wakuu wengine wa nchi wanachama
waliohudhuria kikao hicho ni Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama, Rais wa
Botswana, Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Rais Jacob Zuma wa Afrika
Kusini, Mfalme Mswati wa Tatu wa Swaziland, Rais Michael Sata wa Zambia na Rais
Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Nchi zilizotuma wawakilishi wakiwemo
mawaziri wakuu na mawaziri wa mambo ya nje ni Tanzania, Congo (DRC), Malawi,
Mauritius, Msumbiji, Seychelles na Lesotho.
Waziri Mkuu ambaye alihudhuria kikao
hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ameondoka Luanda, Angola leo asubuhi (Jumamosi,
Juni 2, 2012) kurejea nchini.
إرسال تعليق