RAI wa Kenya, Joshua Mulundi (21), jana alasiri alifikishwa kwa siri
kubwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa
na makosa ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Wakili wa serikali, Ladslaus Komanya, mbele ya Hakimu Agnes Mchome,
alidai kuwa Mulundi ambaye mkazi yake ni Murang’a nchini Kenya, anadaiwa
kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk.
Ulimboka.
Katika shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni 26 mwaka huu, akiwa
katika eneo la Msitu wa Mwabepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha
sheria, mshtakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
Hakimu Mchome alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwani Mahakama
Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Mulundi alidai kuwa kosa aliloshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hata hivyo, Hakimu Mchome alimwambia kuwa shauri hilo linasikilizwa
Mahakama Kuu na siyo mahakamani hapo. Kesi imeahirishwa hadi Agosti 5
mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerejeshwa
rumande.
Juni 27 mwaka huu, Dk. Ulimboka aliokotwa na msamalia mwema katika
msitu huo wa Mwabepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza
kutibiwa.
Lakini hata hivyo, siku chache baadaye madaktari waliokuwa wakimtibu
walisema wameshindwa kumtibu katika hospitali hiyo kwa sababu hakuna
vifaa, hivyo wakamsafirisha kwenda nchini Afrika Kusini ambako hadi sasa
anaendelea na matibabu.
Kova aleza alivyonaswa
Mapema Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alisema kuwa mtuhumiwa huyo Joshua Gitu Mhindi, ana kitambulisho cha
utaifa Na.29166938 kilichotolewa Nyeri na hati ya kusafiria ya dharura
Na.0123431 iliyotolewa Namanga Kenya.
Alisema kuwa katika mahojiano na polisi, mtu huyo alieza kwamba yeye
ni mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama Gun Star
chenye makao yake eneo la Ruiru Wilaya ya Thika nchini Kenya na kudai
kuwa kinaongozwa na mtu mwenye jina la utani Silence akisaidiwa na Past,
ambao wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini Kenya.
Kova alisema kuwa mtu huyo alipohojiwa zaidi alisema alikuja Tanzania
na wenzake 12 kwa lengo la kumdhuru Dk. Stephen Ulimboka baaada ya
kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina, ambaye anaamini kuwa ni mtumishi
wa serikali.
Madaktari waridhia maandamano
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesema maandamano yao yako pale
pale na yatafanyika Jumatatu ya Julai 16, saa nne, na si vinginevyo.
Aidha, MAT, kimelaani kutekwa na kupigwa kwa mwenzao Dk. Steven
Ulimboka na kufutiwa leseni kwa wanafunzi wa vitendo (interns).
Uamuzi huo wa MAT, ulitolewa jijini Dar es Salaam jana, katika kikao
cha dharula cha madaktari 500 walioketi katika ukumbi Kituo cha
Utamaduni wa Korea.
MAT, kupitia Katibu wake, Rodrick Kabangila alisema kuwa kwa pamoja
wanalaani vitendo vya unyanyaswaji wa serikali dhidi yao, uamuzi wa
Baraza la Madaktari (MCT) wa kuwafutia leseni wanafunzi wa vitendo bila
kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kutoa maelezo yao.
“MCT lilishindwa kuwaita na kupata maelezo yao badala yake
walijichukulia hatua za haraka za kuwafukuza, wakati suala hilo lipo
mahakamani,” alisema.
Kwa mujibu wa Kabangila, madaktari wanalaani hatua ya kunyimwa chakula
na kufukuzwa na FFU kwenye vyumba vya kulala (hosteli), madaktari kabla
ya taarifa ya maandishi kutoka wizarani.
Pia wanafunzi hao na wengine walinyimwa posho kabla ya barua ya Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwamba vitendo hivyo na vingine vinaonyesha
udhalilishwaji mkubwa kwao, ikizingatiwa kuwa ni wanataaluma
wanaohitajika ndani ya nchi.
Katika maelezo yake, taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa, na ikiwa
unyanyasaji huo utaendelea, kutasababisha idadi kubwa ya madaktari
kuondoka nje ya nchi.
Alionya kwamba endapo wataondoka taifa litakosa madaktari na kutafanya wananchi zaidi ya milioni 12 kukosa huduma ya afya.
Mbali na hilo, katibu huyo alisema bado milango iko wazi kukutana na
serikali ili kukaa mezani kwa lengo la kumaliza mgogoro wao ambao
umedumu kwa muda mrefu sasa.
Kimsingi, Kabangila alisema kutokana na hatua hizo, wameandaa maandamano pindi watakapopata kibali kutoka vyombo vya usalama.
Hata hivyo, alisema maandamano ni haki yao na kibali ni kwa ajili ya
ulinzi wao; kwamba maandamano yana lengo la kupinga dhuluma na uonevu
dhidi ya taaluma muhimu ya udaktari na madaktari wenyewe.
“Maandamano yataanzia nje ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, tutaishia
kwenye geti la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, tukiwa na mabango ya
kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye Msitu wa
Pande alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka,” alisema.
Dk. Kabangila alisema kuwa wataishinikiza serikali iunde tume huru kwa
ajili ya kuchunguza suala la Dk. Ulimboka itakayofanya kazi haraka na
wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria
Chanzo;- Tanzania Daima
إرسال تعليق