WAKATI michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ikitarajiwa
kuanza leo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro
imekabidhi vifaa kwa timu za Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, mabingwa watetezi Yanga,
wataanza kampeni yao kwa kucheza na mabingwa wa Burundi, Atletico.
Mechi hiyo ya kundi C, itakayochezwa kuanzia saa 10 jioni,
itatanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo kati ya APR ya Rwanda na
Wau Salaam, mabingwa wa Sudan Kusini.
Akizunguza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama
vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicolas Musonye alisema,
wanaamini timu zote 11 zitashiriki.
Alisema hadi jana mchana timu tisa zilikuwa zimewasili huku Tusker ya
Kenya na Ports ya Djibouti zilitarajiwa kuwasili jana jioni.
Alisema timu zote shiriki zimepangiwa viwanja vya mazoezi na hoteli
kwa wakati wote wa michuano hiyo itakayofikia tamati Julai 28.
APR ya Rwanda itakuwa ikifikia Marriot Hotel ya Mabibo External na kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Mabibo Hostel.
AS Vita ya Congo iliyofikia Hoteli ya Chichi, itakuwa ikijifua Uwanja wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
Nayo Atletico ya Burundi, iliyofikia Lunch Time Hotel iliyoko Mabibo, itakuwa
ikifanya mazoezi Uwanja wa Mabibo Hostel.
Aidha Azam ya Tanzania itakayotumia hosteli
yake ya Azam Complex, pia itakuwa ikiutumia uwanja wake wa Chamazi
huku Wau Salaam ya Sudan Kusini itakayokuwa Hoteli ya Rungwe, Kariakoo
itakuwa ikijifua Uwanja wa Sekondari
ya Zanaki.
Mafunzo ya Zanzibar itakayokuwa kwenye hoteli ya Rombo Green View,
Sinza, itakuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi kama ilivyo kwa
Ports ya Djibouti.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba, wao watakuwa kwenye Hoteli ya Vina,
Mabibo Makutano, lakini itakuwa haina uwanja maalumu wa mazoezi kama
watani wao Yanga.
Tusker ya Kenya itakayokuwa kwenye Hoteli ya Rungwe, Kariakoo, itakuwa ikijifua Uwanja wa Zanaki Sekondari.
URA ya Uganda, itakayokuwa kwenye Uwanja wa Sekondari ya Loyola, itaishi kwenye hoteli ya Valentino Royal, Kariakoo.
Nayo taasisi isiyo ya kiserikali ya United Against Malaria (UAM),
inayosimamia mapambano dhidi ya malaria, imejitosa kwa mara ya tatu
kufanya kazi na Cecafa.
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Uam, Fauziyat Abood, wameamua hivyo
wakimiani michuano hiyo itasaidia kufikisha ujumbe wao wa mapambano
dhidi ya malaria.
Kuhusu vifaa kwa Simba na Yanga, Kaimu Meneja wa bia ya Kilimanjaro
inayodhamini timu hizo, Oscar Shelukindo, alisema ni sehemu ya mkataba
wao.
Alisema, Simba na Yanga ni timu kubwa katika ukanda wa Cecafa, hivyo
zinapaswa kutumia vema uenyeji wao kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Vifaa hivyo ni mabeki, vikinga ugoko, viatu, soksi, jezi za mazoezi, mipira na vinginevyo.
Akipokea vifaa hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Simba Geofrey Nyange
‘Kaburu,’ aliishukuru TBL kwani vifaa hivyo vitawafanya washiriki vema.
Naye Hafidh Saidi aliyepokea vifaa kwa niaba ya Yanga, alishukuru na
kuahidi kuonyesha soka maridadi, lengo ni kutetea ubingwa wa michuano
hiyo
إرسال تعليق