WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) sasa wamedhihirisha wazi kuwa kero kwa uongozi wa Bunge.
Hali hiyo imedhihirika waziwazi juzi baada ya kiti cha Spika kuchukua
uamuzi mzito dhidi ya wabunge wawili machachari wa CHADEMA, Tundu Lissu
na John Mnyika.
Juzi kiti cha Spika kilichukua uamuzi mzito dhidi ya hotuba kali ya
kambi ya upinzani ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria
iliyowasilishwa bungeni mjini hapa na mnadhimu mkuu wa kambi ya
upinzani, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu
Lisu na kusababisha kiongozi huyo kupelekwa kwenye Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mnadhimu huyo kukataa kufuta maneno
aliyoyaandika na kuyasoma katika hotuba yake ambayo yalikuwa yakieleza
kuwa baadhi ya majaji wanaoteuliwa hawana uwezo, hivyo wanashindwa
kufanya kazi zao ipasavyo.
Imedaiwa kuwa maneno hayo ni ya kashfa kwa majaji na serikali kwa ujumla.
Awali baada ya kumalizika kwa hoja za wabunge waliokuwa wakichangia
mjadala wa bajeti ya Sheria na Katiba iliyojadiliwa kwa siku moja na
kupitishwa jana. Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Muhagama, alimpa nafasi
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ili kuzungumza kuhusiana
na kauli zilizotolewa na kiongozi huyo wa kambi ya upinzani.
Mwanasheria huyo alieleza kuwa ana wajibu wa kuwaelekeza mawakili
popote walipo na hasa walioko bungeni kufuata na kusimamia misingi ya
taaluma hiyo bila kuathiri wadhifa wao wa ubunge.
“Kwa kweli nimefedheheka sana na maneno yaliyotolewa bungeni leo na
jambo la kwanza ni maoni ya msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kuhusiana
na bajeti ya Katiba na Sheria,” alisema Werema.
Aidha, Werema alitumia nafasi hiyo kumtaka mnadhimu huyo wa kambi ya
upinzani kufuta maneno yake hayo ambayo alisema kuwa hayana ukweli
wowote kwani majaji wote wanaoteuliwa wana uwezo mkubwa na wanateuliwa
kwa kufuata misingi na taratibu husika ambazo zimewekwa za kuwapata
majaji.
“Kauli hiyo ni ya ajabu sana na sikutegemea mtu kama Lisu unaweza
kuzungumza kauli kama hiyo na kuwataja watu ambao hawana uwezo wa
kuingia humu ndani ya Bunge kujitetea huku ukijua dhahiri kuwa kanuni
zetu zinakataza kuwataja watu wa aina hiyo.
“Mwenyekiti namtaka mbunge afute kauli yake hiyo na vinginevyo kama
akikataa basi inabidi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya Mwanasheria Mkuu kutoa muongozo huu kwa mwenyekiti wa Bunge,
shughuli za kupitisha bajeti ya Katiba na Sheria ziliendelea na
zilipomalizika mwenyekiti alimtaka afute maneno yake kama alivyoagizwa
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya kukataa kufuta mwenyekiti
huyo alisema jambo hilo analipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge ili liweze kuchukuliwa hatua.
“Naiagiza kamati hiyo ipitie mwenendo wa shughuli zote kwa siku ya
juzi, pamoja na “Hansard’’ na mtiririko wote wa miongozo iliyotolewa na
kulishauri Bunge nini lifanye katika hatima ya jambo hilo, kwa kufanya
hivyo tutajenga heshima ya Bunge katika kufanya maamuzi na kushughulikia
mambo mengine,” alisema Mhagama.
Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alisema kwenye ukurasa wa tisa wa
hotuba ya kambi ya upinzani Lissu alitamka kuwa kuna baadhi ya majaji
ambao waliteuliwa na rais hawana uwezo na hawakufanyiwa usaili.
Mwenyekiti huyo alisema kauli hiyo inaingilia mambo ya mhimili
mwingine ambao ni Mahakama, hivyo ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Alisema pia kwa kuondoa maneno hayo kutalinda heshima ya uteuzi wa
majaji uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni pamoja na kuwatendea
haki majaji hao kwa kutoendelea kuvunja kanuni namba 64 kwa kujadili
mwenendo wa majaji hao ndani ya Bunge.
Baada ya Mhagama kutoa nafasi hiyo Lissu alianza kwa kukilaumu kiti
kwa kukiuka kanuni na kudai kuwa wanaotaka kutoa maneno hayo katika
hotuba yake hawakuzingatia kanuni.
“Mwenyekiti kwa heshima kubwa sana nimeshangazwa sana na utaratibu
ambao unataka kutumika hapa, kwani haupo katika kanuni za Bunge na haupo
mahali popote,” alisema.
Lisu alisema kama kuna jambo ambalo mtu hakulipenda ama kama amesema
kitu ambacho si cha kweli alipaswa kuomba utaratibu kwa mujibu wa kanuni
68 (1) ili akae na anielekeze kama nilichosema kipo kinyume na
utaratibu na si vinginevyo.
Mnadhimu huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa kama alisema uongo
utaratibu wa kanuni upo kwenye kanuni ya 63, ambayo inazungumzia
kutosema uongo bungeni na hatua za kuchukuliwa dhidi ya mtu huyo na si
kutakiwa afute bila kufuata kanuni kama ilivyo hivi sasa.
“Sasa natakiwa nifute tu bila kufuata kanuni, hapa tutagombana sana na
kwa kitendo hicho cha kuniambia nifute bila kiti chako kufuata kanuni
ni kuniambia mnataka kukanyaga kanuni za Bunge hili, hivyo mimi sitakuwa
tayari,’’ alisema Lissu.
Kwa upande wa Mnyika, Naibu Spika Job Ndugai alilazimika kuagiza
mbunge huyo afikishwe katika kamati hiyo kwa madai ya kutoa tuhuma za
uongo dhidi ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba akidai kuwa
anakabiliwa na tuhuma za EPA.
Agizo hilo hata hivyo lilipingwa vikali na Mnyika pamoja na kambi ya
upinzani, likihoji maamuzi ya kiti hicho juu ya suala hilo.
Mara kadhaa wabunge wa CHADEMA na wale wa NCCR Mageuzi, wameshambuliwa
vikali na wabunge wa CCM, huku ikidhihirika kutetewa kwa nguvu kubwa na
kiti cha Spika.
Mathalani, wabunge wa CCM wamekuwa wakishambulia wale wa upinzani kwa
maneno ya kudhalilisha, lakini kiti cha spika kimekuwa mara kadhaa
kikifumbia macho, kinyume cha hali inapokuwa hivyo kwa wabunge wa
upinzani.
Itakumbukwa kwamba wakati Mnyika akichukuliwa hatua hiyo, hadi sasa
mwongozo wa spika kuhusiana na kauli ya waziri mkuu kulidanganya Bunge,
na lile sakata la Zitto dhidi ya Mkulo havijachukuliwa hatua yoyote kwa
mwaka sasa.
Chanzo:- http://freemedia.co.tz

إرسال تعليق