Hakuna fedha safari za Rais zilizoibwa - Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema uchunguzi wa mwanzo umebaini Sh3.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya safari za Rais ndani na nje ya nchi, zipo salama hazijaibwa.
Akifungua Baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo, kujadili bajeti ya Mwaka 2011/12 na 2012/13 jana, Membe alisema kilichojitokeza ni kasoro na taratibu za fedha zilikiukwa na hakuna dalili zozote za wizi.
“Mwezi wa tatu kwa kipindi cha wiki moja ziliingia fedha nyingi sana katika wizara yetu, ambazo zilizokuwa za safari za Rais tulivyoona hivyo tukazizuia kutumika,” alisema Membe.
Membe alisema baada ya kamati aliyounda kumaliza uchunguzi wa mwanzo, ameiagiza kumaliza kazi hiyo mapema iwezekanavyo ili kubainisha kasoro zilizojitokeza.
“Kasoro hizo tutakapozibaini tutatoa barua za karipio kali kwa wahusika, hivyo wafanyakazi wa wizara yangu kuweni na amani kwani hakuna aliyehusika,” alisema Membe.
Fedha zinazochunguzwa ni zile zilitolewa kati ya Machi Mosi na 8, mwaka huu kwa ajili ya safari za Rais kwenda Geneva nchini Uswis, Brazil, Adis Ababa na Arusha.
Kauli ya Membe inakuja kipindi ambacho kumekuwa na taarifa kwamba, fedha zilizotolewa kutoka Hazina ni Sh3.5 bilioni, wakati zilizokuwa zimepangwa kwa safari hizo ni Sh2 bilioni.Fedha hizo zinadaiwa kutolewa Hazina na maofisa waliokuwa wakikaimu nafasi mbalimbali kwenye wizara hiyo kwa ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 18, mwaka huu, Waziri Membe alisema wakati tukio hilo likitokea, yeye na naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mhasibu Mkuu, walikuwa safarini na kwamba nafasi zao zilikuwa zinakaimiwa.
Kuhusu Balozi

Waziri Membe alisema ili kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa, Balozi zilizopo kwenye nchi mbalimbali zitatumika kuwachunguza watu wanaoomba visa ya kuja nchini.
“Sasa hatutasubiri kumkagua mtu anapofika uwanja wa ndege na kitakachokuwa kikifanyika, ni Balozi zetu sasa zitakuwa chujio la kuchuja wale wote wanaoomba visa ya kuingia nchini kwetu,” alisema Waziri Membe.
Mapendekezo haya nitayapeleka Baraza la Mawaziri kwa lengo la kupitisha pendekezo hili ambalo litasaidia kupunguza wahalifu wanaoingia nchini kinyume na taratibu.
Uwajibika kazini
Waziri Membe aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa umakini na ushirikiano, ikiwamo kuwapa nafasi vijana kwenda balozi za nje kupata uzoefu zaidi.
“Zinapotokea nafasi za kwenda nje tusipendeleane, vijana wanatakiwa kupewa kipaumbele ili waende wakapate mazoezi na sio kwenda walewale,” alisema Membe.
Waziri Membe aliwataka wajumbe wa kikao hicho kupitia bajeti ya mwaka 2011/12, pale ambako kuwalikuwa na changamoto ili kuhakikisha hazijirudii mwaka huu wa fedha.

Post a Comment

أحدث أقدم