Jaji Warioba: Msing’ang’anie kujadili madaraka ya Rais

*Awataka wananchi watoe maoni kuhusu miiko,maadili
*Awamwagia sifa TAHLISO, asema kazi imeanza vizuri
MWENYEKITI wa Tume ya Kukusanya maoni ya Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba amewataka wananchi kuacha kung’ang’ania mabadiliko ya muundo wa uongozi wa madaraka ya Rais na badala yake, wazingatie kutoa maoni kuhusu miiko ya maadili ya kisiasa na kiutamaduni ambayo kwa sasa yanaonekana ni doa kubwa kwa taifa.
Mbali ya kauli hiyo, Jaji Warioba alisema tume hiyo haiko tayari kunyoshewa kidole kama Katiba mpya ijayo, itaonekana kuwa na kasoro ambazo wananchi wanazikataa.

Jajji Warioba, alitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam jana, wakati akifunga kongomano la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (TAHLISO).

Alisema kuna maeneo muhimu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa kwa undani katika Katiba mpya, kwani ndiyo yanayojenga nidhamu, maadili ya taifa kwa wananchi na utamaduni.

“Wananchi lazima wawe makini watoe mawazo mazuri ambayo tutayafanyia kazi na hatimaye kuwa chimbuko la kupata Katiba mpya nzuri na yenye kujenga nidhamu miongoni mwa viongozi wetu,… nawaomba sana wazungume lugha moja tofauti na ilivyo sasa, wote tumeshuhudia namna ambavyo kumekuwa na tatizo la kuporomoka kwa maadili,”alisema Jaji Warioba.

Alisema madhumuni ya tume yake, ni kuona wananchi wanazungumzia ndoto zao katika makundi ya rika mbalimbali ili kupata mwongozo wa taifa la kesho.

“Nimefurahi sana ndugu zangu wa TAHLISO, kuamua kulivalia njuga suala la Katiba mpya na kuichambua kwa kina …nina imani hata kipengere cha haki za binadamu na wajibu wa jamii ni muhimu kinatakiwa kiangaliwe kwa upana ili kieleweke na kuondoa tofauti za sasa,”alisema Warioba.

Alisema awali walikuwa na wasiwasi kutokana na kazi waliyopewa, lakini tangu waanze kazi hiyo Julai 2, mwaka huu (juzi), wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wananchi wengi kujitokeza na kueleza jambo gani wanataka liwe kwenye Katiba mpya.

Alisema tume hiyo, ina makundi saba na wameanza mchakato wa kukusanya maoni katika mikoa mbalimbali, huku akiwaonya vikundi au watu wanaopita katika mitaa kuwafundisha watu cha kuzungumza jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa kongamano hilo walitoa maoni yao juu ya madaraka makubwa aliyonayo Rais na Yutaka yapunguzwe.

Walisema kitendo cha baadhi ya viongozi waliobwagwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, wengi wao wameonekana kupewa nafasi za madaraka ya juu serikalini.

Waliitaka Serikali kuamua muundo mpya wa Katiba ambayo itatumia Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuondoa katiba mbili zilizopo hivi sasa.

Naye, Mwandishi wa Sheria kutoka Zanzibar, Hassan Khaji ambaye ni mjumbe wa tume hiyo, alihimiza umuhimu wa kula kiapo na Watanzania kupata Katiba Marini.

Naye Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa kongamano hilo, aliwapongeza wanafunzi kwa hatua waliyofikia ya kuamua kuichambua Katiba ya sasa na kupata hamu ya kutoa elimu kwa jamii.

Alisema TAHLISO ni kiungo muhimu katika jamii na inatakiwa iungwe mkono kwa ajili ya maslahi ya taifa na jamii kwa ujumla

Post a Comment

أحدث أقدم